HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 31, 2023

WATENDAJI WALIOKAA MUDA MREFU PANGANI KIKWAZO CHA MAELENDELEO-DC ZAINABU

 Na Mashaka Mhando, Pangani

MKUU wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Mohamed, amekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Wizara husika, kuwahamisha watumishi waliokaa muda mrefu katika wilaya hiyo wanaokwamisha Maendeleo.



Akizungumza katika mkutano mkubwa ulifanyika katika uwanja wa sokoni ambao mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman Abdalah, mkuu huyo wilaya alisema kukaa kwao muda mrefu kumewafanya kutotimiza majukumu yao ipasavyo.

Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapa fedha nyingi katika miradi mbalimbali ikiwemo elimu shilingi bilioni 1.6, afya shilingi bilioni 1.8, barabara shilingi milioni 800 na katika sekta ya maji Wizara ambayo inaongozwa na mbunge wa Pangani, serikali imeleta kiasi cha shilingi bilioni 175 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji wa miji 28 ambao mkoa wa Tanga zitahusika wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani.

Alisema pamoja na jitihada nzuri za Rais, alikiri akiwa msimamizi wa shughuli za serikali Pangani kuna changamoto za baadhi ya watumishi hawatekelezi majukumu yao na badala yake wamekuwa wakifanya kazi zao binafsi za kusimamia bodaboda na vibanda vya tiGO Pesa.

"Mheshimiwa Mwenyekiti changamoto ya pili ni serikali kuwaleta watumishi walioharibu sehemu nyingine wanaletwa hapa. Pangani siyo sehemu ya majaribio, tunataka watumishi wenye utayari wa kuwahudumia wananchi na kusikiliza kero zao, lakini siyo kuwa na watumishi wasiotekeleza wajibu wao," alisema.

Hata hivyo, alisema ,akiwa msimamizi mkuu wa shuguli za serikali hatafanya mzaha na mtumishi yeyote ambaye atakayerudisha nyuma Maendeleo ya wananchi na alisema atampatia majina ya watumishi hao wanaoshindwa kwenda na kasi ya Maendeleo ya wilaya hiyo kwa sasa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa, alisema kuwa Pangani ile ya zamani siyo ya sasa, pangani ya sasa inapiga hatua za Maendeleo tangu mbunge Jumaa Hamidu Aweso awe mbunge ambapo serikali imekuwa ikileta fedha nyingi za Maendeleo.



"Pangani tulichelewa sana kimaendeleo lakini tangu awepo mbunge Awesso tumekuwa tukipiga hatua kimaendeleo na mheshimiwa Rais amekuwa akituletea fedha nyingi ni lazima tuzisimamie vizuri ili Maendeleo tunayoyataka yapatikane," alisema Mwenyekiti huyo.

Alisema alipokuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo mambo yakimshinda alikuwa akiyawasilisha mkoani lakini sasa kwa kuwa yupo mkoani atayawasilisha kero zote katika ngazi ya Taifa.



No comments:

Post a Comment

Pages