Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) akisaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Agricom, Alex Duffar, kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji na manunuzi ya pembejeo bora za kilimo kwa wateja wa NMB, hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Fedha wa Agricom, Paul Shayo, kulia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara NMB, Nsolo Mlozi na anayeshuhudia katikati ni Meneja wa Sheria NMB, Jeska Kabisa. (Na Mpiga Picha Wetu).
Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (katikati) akibadilishana hati za mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Agricom, Alex Duffar, kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji na manunuzi ya pembejeo bora za kilimo kwa wateja wa NMB baada ya kuutilia saini katika hafla iliofanyika makao makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa Fedha wa Agricom, Paul Shayo, kulia ni Meneja wa Sheria NMB, Jeska Kabisa na wa pili kulia ni Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara NMB, Nsolo Mlozi. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA MWANDISHI WETU
KATIKA kukuza mchango wa Sekta ya Kilimo kwa Pato la Taifa na kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa mkulima mmoja mmoja na wadau wa mnyororo huo wa thamani, Benki ya NMB imesaini makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya Agricom, yatayowawezesha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa kukopeshwa Matrekta, Zana za Kilimo na Pembejeo nyinginezo.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika jijini Dar es Salaam Jumanne Juni 27, ambapo NMB kupitia Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, imesema ushirikiano huo ni muendelezo wa benki yake kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hasaan ya kuboresha Sekta ya Kilimo iliyoajiri wafanyakazi takribani asilimia 70, na kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 30.
Alibainisha kwamba, wanajivunia ushirikiano huo na Agricom, na kwamba wamejipanga vya kutosha kuibeba Sekta ya Kilimo, yakiwemo mazao ya kimkakati, na kuwa tayari benki yake imeonesha kwa vitendo dhamira yao ya kukwamua wakulima na wadau wake, kwa kuunda Idara Kamili ya Kilimo kwenye taasisi hiyo ya fedha, pamoja na uwepo wa Idara ya Utafiti, zote zikilenga kuunga mkono Serikali.
"Serikali umefanya jitihada kubwa katika sekta hii, nasi tunasaini makubaliano ikiwa ni kuitikia wito huo ambao unadhihirisha namna Kilimo kilivyo kipaumbele cha Serikali yetu Ili kutanua WiGo wa Sekta ya Kilimo kuchangia Pato la Taifa.
"Lengo la ushirikiano huu ni kukuza na kuleta mabadiliko ya kilimo kwa wakulima wa kada zote, kupitia makubaliano haya wakulima watapata mikopo ya Matrekta, Zana za Kilimo na Pembejeo - huruma ambazo zinatokewa na washirika wetu hawa wa Agricom.
"Msukumo wa yote haya ni NMB kutambua umuhimu wa sekta hii kwa Uchumi Endelevu wa Taifa," alisema Mponzi huku akibainisha kuwa, wakulima watakaokopa zana ama Pembejeo hizo za Kilimo, watalazimika kuwa na asilimia 20 tu ya malipo ya awali.
Aliongeza ya kwamba NMB italipia asilimia 80 inayobakia na mkopaji atakuwa huru kulipia marejesho ya mkopo kwa msimu wa zao husika ama kulipa kwa mikupuo tofauti kutoka katika vyanzo vinginevyo, huku akiwataka wadau kujitokeza kwenye matawi 229 ya benki hiyo kote nchini, kupata huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Agricom Africa, Alex Duffar, alikiri kufurahishwa na kusainiwa kwa makubaliano hayo baina ya NMB na taasisi yake aliyoitaja kama kinara wa mauzo ya Zana Bora na za Kisasa za Kilimo, na kwamba ukubwa wa washirika hao, unaenda kuinua wakulima na kusukuma mbele maendeleo ya Sekta ya Kilimo Tanzania.
Duffar alibainisha kuwa, Kampuni ya Agricom ina masuluhisho mengi yanayokidhi mahitaji ya wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo, walikobobea katika uzalishaji wa Pembejeo na zana muhimu zinazokidhi hatua zote muhimu za kilimo, ikiweko utayarishaji wa ardhi na umwagiliaji, upandaji, upaliliaji, utunzaji wa mazao na uhifadhi wake baada ya mavuno.
Aliongeza kwamba ushirikiano baina yao unaojumuisha Wateja wadogo, wa kati na wakubwa zaidi ya 7000, na NMB iliyo na mtandao mpana wa matawi kote nchini, unalihakikishia Taifa ukuaji wa haraka wa Sekta ya Kilimo na Uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, huku akibainisha kwamba Agricom iliyoanzishwa mwaka 2009, inao wauzaji walioidhinishwa zaidi ya 40 na matawi yapatayo 13 - wote wako wa tayari kuhudumia wateja wa NMB watakaohitaji mikopo.
"Tunajivunia mashirikiano haya baina ya taasisi vinara, Sisi tukiwa na mtandao mkubwa wa Wateja na matawi mengi, kama ilivyo kwa NMB ambayo imesambaza matawi kote nchini. Ni ushirikiano unaolihakikishia Taifa tija, kama tulivyothibitisha kupitia bidhaa zetu kwa wakulima wa mazao ya mpunga, pamba, tumbaku, kahawa na mengineyo.
"Ushirikiano wetu huu na NMB ni muendelezo tu, tumefanya mengi pamoja na tunaamini makubaliano haya Sasa yanaenda kunufaisha Wateja wa pande zote mbili, kwani tunaamini katika ubora wa bidhaa zetu na telnolojia iliyotumika katika utayarishaji wake," alisema Duffar.
Awali, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara (Agri - Business) wa NMB, Nsolo Mlozi, alisema benki yake imefanya uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Kilimo, ilikotoa mikopo ya mabilioni kwa wadau, lengo likiwa ni kusapoti ustawi wa sekta hiyo nchini, huku akiwataka wakulima kuchangamkia mikopo hiyo ya Matrekta, Zana na Pembejeo za Kilimo, kwani Kilimo kinakosa tija iwapo kitafanywa bila zana na pembejeo bora na za kisasa.
No comments:
Post a Comment