HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 07, 2023

RC SINGIDA ARIDHISHWA NA UTEKELEZWAJI WA MIRADI WILAYA YA IKUNGI


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati), akizungumza wakati alipokuwa akiukagua mradi wa maji katika Kijiji cha Matare uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi wakati wa ziara yake aliyoifanya leo Juni 6, 2023.

......................................................

Na Dotto Mwaibale, Ikungi

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba  amefurahishwa na kuridhishwa na usimamizi mzuri na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na kuwapongeza viongozi wote kwa utekelezaji wa miradi hiyo kwa thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Serukamba  ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake wilayani humo aliyoifanya leo Juni 6, 2023 ambapo alipata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhimiza ikamilike kabla ya Julai 1, 2023.

Aidha, Serukamba amewapongeza wataalam na wananchi kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia utalaam na nguvu kazi katika kutekeleza miradi hiyo ambayo imegharimu fedha nyingi.

"Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii naomba tumuheshimishe Rais wetu kwa kuikamilisha haraka kabla ya Julai 1, 2023 ili ianze kutumika," alisema Serukamba.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa ikimpa raha kutokana na kufanya vizuri katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuwa imekuwa ikipata mafanikio hayo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya viongozi, wataalam na wananchi.

Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni mradi wa maji katika Kijiji cha Matare uliopo Kata ya Unyahati uliogharimu Sh. Milioni 386.8 ambao utawahudumia wananchi 5036, ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Matare na ujenzi wa mabweni mawili na bwalo katika Shule ya Msingi  Ikungi.

No comments:

Post a Comment

Pages