Na Farida Ramadhani-Dodoma
Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewaagiza wataalamu
wa Wizara ya Fedha na Mipango na ujumbe kutoka Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF), kujadili namna ya kushughulikia athari za upungufu wa
dola za Kimarekani katika mzunguko wa fedha ili kunusuru uchumi wa nchi
zinazoendelea.
Mhe. Dkt. Nchemba (Mb) ametoa
maagizo hayo wakati wa kufungua kikao kilichowashirikisha wataalam
kutoka Shirika la Fedha na Kimataifa (IMF) waliowasili nchini kwa ajili
ya kufanya tathimini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), kwa
kushirikiana na wataalam wa ndani wa Serikali.
Alisema
mabadiliko ya Sera za Fedha nchini Marekani ya kubana matumzi na
kupunguza dola kwenye mzunguko wa fedha, yameleta athari zinazoonekana
mpaka kwenye nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Tumekuwa
tukirejea Uviko na vita baina ya Urusi na Ukraini kama moja ya vitu
vinavyoathiri uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania lakini
upungufu wa dola unaathiri uchumi kwa kiwango kikubwa ikiwemo uagizaji
wa mafuta na uagizwaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika katika shughuli
za Sekta Binafsi”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema
ni vema kutafuta namna ya kushughulikia jambo hilo kisera ili kunusuru
nchi zinazoendelea kwa kuwa sekta ya nje ni muhimu katika kuchochea
ukuaji wa uchumi wa ndani.
Kwa upande wake
Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw.
Harris Tsangaride, alisema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na
Tanzania ili kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua kiuchumi na
kijamii.
Aliipongeza Serikali kwa Sera zake nzuri ambazo
zinaendelea kutekelezwa katika kukabiliana na athari za vita ya Ukraine
na kuongeza kuwa ni matarajio yao kuwa zitaendelea kuchokea ukuaji wa
uchumi na maisha ya wananchi.
Bw. Tsangaride
alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache katika kanda ambazo
zinafanya vizuri katika kutekeleza programu mbalimbali kwa kushirikiana
na Shirika hilo na hivyo katika kikao hicho watajadiliana namna bora ya
kuendelea kuiona nchi ikifanya vizuri zaidi.
No comments:
Post a Comment