HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 10, 2023

Watetezi haki za wanawake washauriwa kuungana

 

Baadhi ya watendaji wa (WGNRR) walioshiriki katika warsha hiyo ya kuwajengea uwezo wanahabari


Ofisa vijana katika programu za afya ya uzazi WGNRR, Walta Carlos, akizungumza katika warsha hiyo wakati akiwasilisha mada.


Na Mwandishi Wetu


WITO umetolewa kwa wadau na watetezi wa haki za binadamu hasa wanawake, kufanya kazi pamoja ili kupaza sauti zao na kuibua chagamoto wanazopitia katika jamii. 


Hayo yamebainishwa leo Juni 9,2023 jijini  Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Shirika la Mtandao wa Wanawake Duniani kwa ajili ya Utetezi wa Haki za Afya (WGNRR), Nondo Ejano wakati akifunga warsha ya kuwajengea uwezo  waandishi wa habari katika masuala ya afya ya uzazi.


Amesema ushirikiano huo utasukuma mbele ajenda mbalimbali kwa serikali na watoa huduma kufanya marekebisho kwenye maeneo tofauti ikiwemo sheria ya ndoa.


"Leo hii tuna mjadala ambao umekuwa ukiendelea kuhusu sheria, hivyo sisi kama wadau ni muhimu kushirikiana kwa kuweka mikakati ya pamoja badala ya kila mtu kufanya kwa namna yake," amesema Ejano.


Mkurugenzi huyo wa WGNRR amesema hakuna nguvu ya kutosha kwa ajili ya waathirika wote katika jamii hivyo uwepo wa nguvu ya pamoja utasaidia kupaza sauti yenye kusikika na kuleta mabadiliko chanya dhidi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za wanawake na afya.


"Vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu ni vingi kama vile ubakaji, shambulio la kigono  vinasababisha athari za kiafya kwenye maisha ya  wasichana na wanawake hivyo basi kupitia kalamu zenu tunaimani kwa pamoja tutaweza kuibua chagamoto hizo," amesema Ajano.


Ajano anaamini ushirikiano huo, utasaidia kusukuma mbele ajenda mbalimbali kwa serikali na watoa huduma kufanya marekebisho kwenye masuala mengine ikiwemo sheria ya ndoa.


Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, WGNRR linatetea upatikanaji wa huduma sahihi na stahiki za afya ya uzazi kwa watu wote.


"Tumekuwa tukifanya kazi na jamii lakini kipaumbele chetu zaidi ni wale watu ambao wako katika hali ya chini lengo letu ni kuhakikisha jamii inapata haki ya kupata huduma stahiki za uzazi wa mpango bila ubaguzi," amesema.


Kwa upande wake Ofisa Vijana katika Programu za Afya ya Uzazi WGNRR, Walta Carlos, amesema katika kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo hivyo, ni muhimu kuwepo kwa ushirikiano wa wadau wote. 


Amesema watu wengi wanapaza sauti zao na kuwasahau afya za wanawake ambao ni muhimu sana katika jamii.


"Masuala ya harakati hizi za afya ya uzazi na haki zaidi kwa wanawake na wasichana ni vizuri wadau wote kwa ujumla kushirikiana kwani tunaaamini vyombo vya habari vina nguvu kubwa... sasa wakishirikiana na taasisi na asasi za kijamii hatimaye kutengeneza mkakati wa pamoja ikiwemo kufanya uchambuzi wa baadhi sera, lazima serikali itasikia na kufanya mabadiliko yanayofaa kwenye eneo hili," amesema Walta.

No comments:

Post a Comment

Pages