HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 21, 2023

Matinyi atoa maagizo mazito soko la Zakhem

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi, akizungumza alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko la Zakhem.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi (kulia), akipata ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, mkoani Dar es Salaam Elihuruma Mabelya (kushoto) juu ya ujenzi wa soko la Zakhem. Katikati ni Katibu wa CCM wilayani humo, Daniel George.


Na Selemani Msuya

 

MKUU wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Mobhare Matinyi ameitaka Kampuni ya Group Six kukamilisha ujenzi wa soko jipya  na la kisasa la lililopo Zakhem kata ya Kibonde Maji wilayani humo,  ifikapo Agosti 15 mwaka huu.

Aidha Matinyi amewataka watendaji na viongozi wa manispaa kuhakikisha mchakato wa ugawaji maduka na vizimba vya biashara uwe umekamilika ifikapo Agosti 31/2023.

DC Matinyi ametoa maelekezo hayo leo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa soko hilo la kisasa lilojengwa katika Manispaa ya Temeke.

Amesema Soko la Zakhem limejengwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan  kwa kutoa  shilingi bilioni 2.843, hivyo kuwataka wafanyabiashara watakaopata nafasi ya kufanya biashara walitunze.

Mkuu wa wilaya huyo amesema kwa mujibu wa taarifa ya mkandarasi ujenzi umefikia asilimia 99.9, hivyo kumtaka ifikapo Agosti 15 mwaka huu awe amekabidhi kwa manispaa ili michakato mingine iweze kuendelea.

"Nimekuja hapa kuangalia maendeleo ya ujenzi wa soko, nimeambiwa ujenzi umefikia asilimia 99.9 nitumie nafasi hii kumuelekeza mkandarasi ifikapo Agosti 15 awe amekabidhi soko na upande wa manispaa wahakikishe mchakato wa ugawaji unakamilika ifikapo Agosti 31, ili biashara ianze kufanyika,"amesema.

Matinyi amesema serikali imedhamiria kuwakomboa wananchi kiuchumi, hivyo ni imani yake kuwa watakaopata nafasi ya kufanya biashara kwenye soko hilo la kisasa watapata maendeleo na kulipa kodi kwa wakati.

Mkuu huyo wa wilaya ameonya watu ambao wanatarajia kupata maeneo ya kufanya biashara katika soko hilo, halafu nao wakodishe wengine kwa bei kubwa.

Kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya Matinyi amewataka wafanyabiashara watakaopata nafasi ya kufanya biashara eneo hilo wazingatie usafi ili kuepusha magonjwa kwa wateja wa bidhaa zao.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya amesema katika soko hilo wanatarajiwa kupangisha wafanyabishara zaidi ya 300 ambapo 150 watakuwa kwenye upande maduka na 160 upande wa vizimba.

Mabelya amesema soko hilo litakuwa na ofisi za mama lishe 20, ambao watatoa huduma ya chakula kwa wafanyabiashara.

"Soko limekamilika kwa asilimia 99.9 tutatoa kipaumbele kwa wafanyabiashara ambao walikuwepo na nafasi zitakazo bakia watapewa wengine kwani maombi ni zaidi 3,800 huku nafsi zikiwa 300," amesema.


Mkurugenzi huyo amesema manispaa inatarajia kuongeza mapato kupitia soko hilo, hivyo kuahidi kuendelea kuboresha masoko mengine.


Aidha, Mkurugenzi Mabelya amewataka wafanyabiashara wanapanga bidhaa barabara kuhamia maeneo ambayo yamerusiwa kisheria na kwamba hawatawavumilia.

Amesema wanajipanga kufanya opersheni saa 24  kuwakamata wale ambao wanakiuka sheria za nchi.

Mabelya amesema yapo maeneo mengi ambayo yametengwa kwa ajili ya biashara, hivyo hawapo tayari kuruhusu biashara zifanyike barabarani.

Halikadhalika mkurugenzi huyo amesema manispaa imetenge shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ukarabati wa masoko ya wilaya hiyo, huku shilingi bilioni 4 zikitegwa kwenye ujenzi wa barabara kwenye mitaa.

Meya wa Temeke Abdallah Mtinika ameshukuru Serikali kufanikisha ujenzi wa soko hilo na kuahidi kulilinda ili liweze kudumu kwa muda mrefu.

Mtinika ambaye ni Diwani wa kata ya Kibonde Maji lilipo soko hilo amesema soko hilo ni mkombozi kwa wananchi wake na Tanzania kwa jumla.

"Nasisitiza kuwa mimi kama meya na diwani wenu wataopata nafasi ni wale ambao walikuwepo na baada ndio hawa wapya," amesema.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel George amesema ujenzi wa soko hilo ni utekelezaji wa Ilani ya chama ambayo inataka Watanzania kuinuliwa kiuchumi na kijamii.

George amesema chama hicho kitahakikisha miradi yote ambayo imeanzishwa kwenye ilani inatekelezwa katika kipindi husika ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi.

No comments:

Post a Comment

Pages