HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 14, 2023

Prof Silayo atangaza fursa ya asali China


Kamishna Mkuu wa TFS, Profesa Do Santos Silayo akisaini kitabu cha wageni katika banda la Wizara ya Maliasili ndani ya viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Ofisa Mhifadhi Mkuu (TFS) Kassim Ally akitoa maelezo kwa Kamishna Mkuu wa TFS, Profesa Do Santos Silayo wakati alipotembelea banda la wakala hiyo ndani ya Viwanja vya Sabasaba. (Picha na Selemani Msuya).


Na  Selemani Msuya 


KAMISHNA wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Do Santos Silayo amewataka Watanzania kuchangamkia fursa ya ufugaji nyuki ili waweze kukidhi hitaji la tani 200,000 kwa mwaka katika soko la China.


Prof. Silayo amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 47 katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.


Kamishna Silayo amesema hali ya ufugaji nyuki na uzalishaji asali kwa hapa nchini bado sio ya kuridhisha, hivyo kuwataka wananchi katika maeneo mbalimbali kuwekeza kwenye eneo hilo kwa kuwa kuna soko la uhakika China na nchi nyingine duniani.


“TFS tunaweka mkazo katika ufugaji wa nyuki kisasa ili kuongeza uzalishaji wa asali, kwani soko lake ni kubwa kuanzia ndani na nje ya nchi, Mfano nchi ya China pekee inahitaji tani 200,000, tunapaswa kuichangamkia fursa hii,” amesema.


Amesema wakala hiyo imejipanga kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu, ikiwemo asali na misitu, hivyo watatoa ushirikiano na mafunzo kwa mtu au kikundi ambacho kinahitaji kufanya shughuli hiyo.


Kamishna huyo alisema wanachopambana nacho kwa sasa ni kuhakikisha bidhaa ya asali ambayo inazalishwa nchini inakuwa na ubora ambao utaleta ushindani katika soko la dunia.
Amesema changamoto katika eneo la asali ilikuwa ni namna ya kufuga, ila kupitia miradi mbalimbali wamekuwa wakiendelea kutoa elimu na matokeo yameanza kuonekana.


Aidha, Kamishna Silayo amesema kutokana na nguvu kubwa ambayo serikali imekuwa ikivutia wawekezaji kumekuwa na ongezeko kubwa la usafirishaji wa mazao ya misitu kwenda nje ya nchi.
“Usafirishaji wa mazao ya misitu nje ya nchi umeongezeka hadi kufikia mita za mraba 95,000 zilisafirishwa, huku tukiingiza 30,000,  zamani tulikuwa tunasafisha mita za mraba 25,000 na kuingia 130,000, yote haya ni kutokana na uongozi mzuri wa Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Halikadhalika Prof. Silayo amesema TFS inahamasisha huduma ya utalii ikolojia ambao unapatikana katika misitu takribani 23 wanayoisimamia hali ambayo itaongeza fedha za kigeni na kukuza uchumi wa nchi.


“Msitu kama Pugu, Kazimzumbwi, Vikundu, Uluguru, Amani, Nilo, Chome, Sao Hill na mingine ambayo kiujumla inafaa kwa utalii kukimbiza magari, pikipiki na mbio zingine,” amesema.
Aidha, amesema katika kupambana na usafirishaji wa mazao ya misitu kama mkaa TFS inashirikiana na mamlaka zingine kuhakikisha kuwa wanaosafirisha ni wale ambao wamekidhi vigezo.

No comments:

Post a Comment

Pages