HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 14, 2023

WAZIRI JENISTA MHAGAMA AIPONGEZA TARURA KWA UFANYAJI KAZI JIMBO LA PERAMIHO

NA STEPHANO MANGO, SONGEA 

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na uratibu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Joakim Mhagama amewapongeza Wakala wa Barabara za vijijini na mijini  Tanzania Wilaya ya Songea(TARURA ) kwa namna wanavyowajali wananchi wa Jimbo la Peramiho.

 

Waziri Jenista Mhagama ametoa pongezi hizo jana wakati akikagua  daraja la Mto Njoka katika Barabara ya Kizuka - Mipeta – Matama - Mhukuru barabarani ambayo  ina urefu wa jumla ya kilomita 63 ambayo inawasaidia wananchi wa kata ya kizuka na kata ya Muhukuru.

 


Alisema kuwa barabara hiyo ni muhimu sana kiuchumi na kiulinzi kwani kata hizo zipo jilani nan chi ya Msumbiji , hivyo kitendo cha Tarura kuzitengeneza barabara na madaraja mara kwa mara pale yanapoharibika kutokana na sababu mbali mbali ni jambo la kuwashukuru sana.

 

Waziri huyo alisema kuwa wakazi wa Jimbo la Peramiho kwa namna ya pekee kabisa wanaendelea kutoa shukran za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za ujenzi wa daraja hili na kuanza kufungua barabara hii muhimu kwenye Wilaya ya Songea.

 

Alisema kuwa barabara hiyo inaunganisha Kata ya Kizuka na Mhukuru ambapo ina Mito mikubwa mitatu (Mgugusi, Njoka na Mhukuru) yenye upana wa zaidi ya mita 20 pia ina mito midogo minane (Dabadaba, Mwangazi, Nakangwiti, Chapanoti, Mipeta, Namahomba, Mkulumo na Ngunguti) yenye upana wa mita 5 mpaka 10. 

 

Akitoa taarifa za ujenzi  wa daraja la Mto Njoka (m20) Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea Mhandisi Johnson  Kweka alisema kuwa mradi huo wenye mkataba Namba AE/092/2022/2023/RVM/W/33 unatekelezwa na Mkandarasi HERA CONSTRUCTION CO. LTD wa Dar es Salaam.

 

Mhandisi Kweka alisema kuwa  ujenzi wa daraja hilo utatumia gharama ya Shilingi Mia Sita Tisini na Tisa Milioni Mia Nane Tisini na Mbili Elfu Mia Nne Sitini na Tano Tu (TZS. 699,892,465.00) ambapo muda wa utekelezaji wa mkataba huu ni miezi 08 kuanzia tarehe 15/12/2022 na unatarajia kumalizika tarehe 15/08/2023.

 

Alisema kuwa hadi hivi sasa fedha zote za utekelezaji wa mradi huu zimeshapokelewa na Mkandarasi hajaomba malipo yoyote ambapo kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mkataba huu wa Ujenzi wa Daraja la Mto Njoka ni pamoja na Kusafisha eneo la ujenzi wa Daraja, Kuondoa miti katika eneo la mradi.

 

Alizitaja kazi zingine ni Kuchimba udongo na kupasua mawe kwa ajili ya ujenzi wa msingi wa Daraja, Ujenzi wa msingi wa Daraja, Ujenzi wa nguzo na mikono ya Daraja,  Ujenzi wa Bimu na Deck,  Ujenzi wa kingo za Daraja,  Kufitisha alama za Daraja,  Uwekaji wa Gabion katika Daraja na Uwekaji wa tabaka za udongo kwenye maingilio ya daraja.

 

Mhandisi Kweka alisema kuwa hadi sasa Mkandarasi ameshatekeleza kazi  ya Kusafisha eneo la ujenzi wa Daraja ,Kuondoa miti katika eneo la mradi, Kuchimba udongo na kupasua mawe kwa ajili ya ujenzi wa msingi wa Daraja na Ujenzi wa msingi wa Daraja.

 

Alisema kuwa Kwa sasa mkandarasi anaendelea na ufungaji wa nondo na boksi kwa ajili ya nguzo na mikono ya daraja ambapo kwa ujumla mradi hadi sasa umefikia asilimia 40 na utekelezaji wa mradi unaendelea.

 

Aidha daraja la mto Mgugusi ndio pekee limebaki na limepangwa kutengewa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/ 2025 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu ili barabara hii iweze kupitika katika kipindi chote cha majira ya mwaka.

 


Mhandisi Kweka alisema kuwa  katika mradi huo walikabiliwa na Changamoto ya mvua nyingi zilizonyesha kuanzia mwezi Novemba, 2022 hadi Mei 2023 hata kusababisha kujaa kwa maji kwenye mto Mgugusi na mto Njoka hali iliyoathiri utekelezaji wa mradi huu kwa kushindwa kufika eneo la kazi na kuanza kwa ujenzi wa msingi wa daraja.

 

Alisema kuwa Tarura inaendelea kufanya  mawasilino ya barabara kati ya kata ya Mhukuru na Kizuka yanaendelea kuimarika kwa kuwa na madaraja ya kudumu kwenye mito minne (Njoka, Namahomba Mkulumo na Ngunguti) ambayo yapo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na kazi ya ufunguaji wa barabara umbali wa km 28 unayoendelea.

 

Mhandisi Kweka alisema kuwa Ofisi ya Meneja Wilaya kwa kushirikiana na watumishi waliopo tutaendelea kutekeleza majukumu ya Wakala kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kufikia lengo la kupunguza kero ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Wilaya ya Songea.

 

 Aidha tunakushukuru Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama kwa kutusaidia kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili na kutatua changamoto za mbali mbali za miundombinu ya barabara iliyopo kwenye Wilaya yetu. Pia tunamshukuru  Diwani wa Kata ya Kizuka kwa ufatiliaji wa fedha hizi, ushauri na ushirikiano katika utekelezaji wa ujenzi wa daraja hili.

 

Vilevile tunaushukuru Uongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea kwa usimamizi na maelekezo ya mara kwa mara unayotoa wakati wote kwani yamekuwa yakitusaidia katika kuhakikisha tunafikia lengo katika majukumu yetu.

No comments:

Post a Comment

Pages