HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 29, 2023

ROBERTINHO AWANG'ATIA MENO WASHAMBULIAJI

Na Mwandishi Wetu 


KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’, ameanza kufanyia  marekebisho safu yake ya mbele kwa kuwafungia kazi mastaa wapya akiwemo Luis Miquissone, Kramo Aubin ,Willy Essomba Onana na Fabrice Luamba Ngoma.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni mara baada ya kikosi chake kucheza michezo mitatu ya kirafiki na Kocha Robertinho kuangalia viwango vya wachezaji wake waliokuwepo msimu uliopita na wapya waliosajiliwa.


Akizungumza na Habari Mseto, Robertinho amesema kazi  atakayoifanya katika kipindi kilichobaki cha maandalizi ya msimu mpya ni kutengeneza muunganiko wa timu kwa kuwa ana wachezaji wengi wapya.


Amesema anataka kuhakikisha nyota wapya wote walioingia kwenye dirisha hili la usajili wanaingia kwenye mifumo na kutengeneza timu yenye uwiano sawa kati ya wale watakaoanza kwenye kikosi cha kwanza na watakaoanzia benchi.


"Nataka kila mchezaji wakiwemo Miquissone na Onana, Ngoma na wengine  wajitume kwa asilimia zote  kupata nafasi, tumesajili wachezaji wazuri kinachofuata ni kutengeneza timu yenye muunganiko imara." Amesema 


Robertinho ana Imani kubwa kuwa muda uliosalia  watafanikisha kupata muunganiko kwa umoja na msimu ujao utakuwa bora zaidi kwao, kwa sababu ya kuridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake licha ya kupoteza mechi moja ya kirafiki kwa bao 1-0 dhidi ya Turan PFK.


“Walicheza vizuri kwenye kushambulia,  kuzuia pamoja na kumiliki mchezo kwa muda mrefu, ubora wa kikosi changu, sasa ninaamini tutafanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mashindano ya ndani msimu mpya wa 2023/24.


"Kwangu siangalii matokeo ya mwisho bali mchezo wenyewe ulivyokuwa , tumecheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho wachezaji wameonekana wapo timamu kimwili , kimbinu na hili ni jambo ambalo limenifurahisha , nawapongeza pia wasaidizi wangu wamefanya kazi kubwa kwa muda mfupi,” amesema Robertinho.


Amebainisha kuwa anahitaji kucheza mechi nyingine moja ya kirafiki mwishoni mwa juma kabla ya timu hiyo kurejea Dar es Salaam katika kukamilisha sherehe za Simba Day na kuendelea na maandalizi ya msimu mpya  wa mashindano yaliyopo mbele yao.

No comments:

Post a Comment

Pages