Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Chuo
Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimewakaribisha wahitimu wa Kidato cha Sita
kutembelea banda la chuo hicho ili waweze kujionea kozi za fani
mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo na kufanya udahili kwa mwaka wa
masomo 2023/24.
Aidha, chuo hicho
kimewasisitiza wahitimu hao kuchangamkia fursa za masomo yanayofundishwa
UDOM kwani watakapojiunga watajengewa maarifa ya kuweza kujiajiri baada
ya kuhitimu masomo yao.
Hayo yamesemwa na
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Lughano Kusiluka katika Ufunguzi wa
Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika
katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa wanafunzi watakaojiunga na UDOM watapata fursa ya kufundishwa fani
mbalimbali kwa umahiri ili kuwajengea hali ya kujiamini pale
wanapohitimu wawe na mawazo na uwezo wa kujiajiri.
"
Tumekuja hapa kwa ajili ya kuwaelimisha wanaotaka kujiunga UDOM
nawakaribisha wanafunzi waje kusoma katika chuo hiki kwani watapata
elimu bora itakayowajengea uwezo wa kufikiria kujiajiri," amesema
Profesa Kusiluka.
Amebainisha kuwa chuo hicho
ni kikubwa na kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 32,000 na kwamba
kimejengwa mahasusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa Watanzania wengi hivyo
wanafunzi wacahangamkie fursa za masomo chuoni hapo.
Amesisitiza
kuwa UDOM kinatoa zaidi ya Progamu 80 katika Ngazi ya Shahda ya Awali
na progarmu zaidi ya 56 kwa ngazi ya Shahada za Umahili huku akibainisha
fani zinazotolewa ni Udaktari, Uchumi, Sheria, Sosholojia, Utawala wa
Biashara, Biashara na Uhasibu, Biashara katika Rasilimali Watu,
Ujasiriamali na Biashara ya Kimataifa.
Nyingine
ni Utalii, Masoko, Mazingira, Takwimu, Ununuzi na Ugavi, Teknolojia ya
Habari na Mwasiliano (TEHAMA), Jiolojia, Kemia, Madini, Petroli,
Nishati Mbadala, Elimu, Lugha, Uhusiano wa Kimataifa, Ikolojia, Uandishi
wa Habari na Mahusiano ya Umma na Fizikia.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Rose
Joseph amewakaribisha wanafunzi kujiunga na chuo hicho kwani kina
mazingira rafiki ya kujisomea watapokuwa chuoni hapo.
Maonesho
hayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo Kukuza Ujuzi nchini
Kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na Uchumi Imara na Shindani
huku yakishirikisha Vyuo Vikuu na Taasisi ya Elimu ya Juu zaidi ya 80
yakitarajiwa kuhitimishwa Julai 22 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment