HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 24, 2023

ZAWA kusambaza huduma ya Maji Safi na Salama kwa njia ya Gari

Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Zanzibar Mhe. Shaaban Ali Othman amesema wizara hiyo kupitia taasisi yake Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) wanajipanga kusambaza huduma ya Maji Safi na Salama kwa njia ya gari la maji katika maeneo ambayo wananchi wamekosa huduma hiyo ikiwemo eneo la Kilimani, Maisara, Michenzani Jumba (block) na namba Kumi.


Kauli hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi wa maeneo  hayo kulalamikia ukosefu wa huduma hiyo tangu kuanza kwa ujenzi wa Mradi wa barabara ya Mnazi mmoja hadi  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Unguja.


Akizungumza katika ziara maalumu iliyoandaliwa jana na Wizara yake katika eneo hilo la mradi wa barabara hiyo, Mhe, Othman amesema katika kipindi hichi atahakikisha ZAWA wanawafikishia  wananchi huduma hiyo kwa njia ya gari la maji bila ya kuwatoza fedha.


“Tutatoa maji bure katika kipindi hichi,narudia tena bure kwa maana ya bure hatutomchangisha mtu pesa, maji tunayo na magari yapo. kwani wizara zote mbili zinafanya kazi kwa mashirikiano makubwa na muda sio mrefu huduma ya maji itarudi kama kawaida, hivyo tutasambaza maji bure” Alisema Othman.


Naye katibu Mkuu wa wizara hiyo Joseph Kilangi amesema ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo hayo umetokana na kuathirika kwa miundombinu ya maji wakati mradi wa barabara ukiendelea hivyo kupitia ziara hiyo imelenga kutafuta majibu ya kujua wapi mabomba ya maji yatapitishwa ili huduma hiyo irudishwe kwa wananchi.


Amesema wizara yake imekubaliana na Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi kupitisha mabomba ya maji pembezoni mwa barabara (walk way) hivyo, muda sio mrefu mradi huo utakamilika na huduma ya maji itarudishwa kwa wananchi kama kawaida.


Aidha katibu Mkuu Kilangi amewaomba radhi wananchi waliyokosa huduma ya maji safi na salama katika kipindi hichi kwani Serikali ya Mapinduzni Zanzibar (SMZ) imejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi wake hivyo Barabara ni muhimu na maji ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake.
.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi Khadija Khamis Rajab amesema wizara yake inafanya kazi kwa mashirika makubwa na Wizara ya Maji, Nishati na Madini hiyo watahakikisha wanarudisha miundombinu ya maji na umeme yote iliyoathirika wakati wa ujenzi wa barabara.


Pia amesema miundombinu ya umeme itakayoathirika itarudisha na taasisi husika Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ili wananchi waendelee na harakati zao za maisha ya kila siku.
Wakati huo huo, akizungumza Mkurugenzi Mkuu ZAWA Mhandisi Dkt. Salha amesema maji yamejaa tele katika tangi la maji la Mnara wa mbao Kilimani, lakini hakuna jinsi  ya  kuwafikishia wananchi kutokana na miundombinu ya maji kuathirika, hivyo taasisi yake inajipanga kuwafikishwa wananchi huduma hiyo kama walivyotoa katika kipindi cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani.


“Taasisi yangu imeshatoa maelekezo dizaini na dayamita (design na diameter) ya mabomba ya maji ambayo Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi watalazimika kununua kwaajili ya kurudisha huduma  hiyo  kwa wananchi kama kawaida” Alisema Mhadis Dk. Salha.


Kwa upande wa wananchi akizungumza Mkaazi wa Kilimani Bi Luluwa Salum Ali (36) ameiomba Serikali mara tu mradi wa barabara utakapo kamilika warudishiwe huduma hiyo kwani hivi sasa wanalazimika kununua gari la maji kwa bei ya Tsh. 15,000 kwa kujaziwa tangi la lita 1500 au kwenda kukaa foleni kwa jirani  ambaye amechimba kisima  huko bei ya kujaziwa tangi la maji la lita 1500 bei ni Tsh. 5000, lakini watu ni wengi lazima mtu apange foleni.


“Siwezi kuilamu Serikali najua tunatengenezewa barabara lakini ninachokiomba kwa mamlaka husika barabara itakapokamilika tu, basi turudishiwa huduma hiyo kwani tumekabiliwa na kipindi kigumu hasa ukiangaliwa tofauti ya kipato kwa wananchi” Alisema Luluwa.

No comments:

Post a Comment

Pages