Akizungumza na wanahabari Jijini humo Mkuu wa Chaneli ya Sinema zetu Sophia Mgaza amesema katika kutimiza msemo wao maarufu wa ‘burudani kwa wote’, Azam TV vinara wa huduma bora za maudhui na burudani za kusisimua nchini, kwa mara nyingine tena wanajivunia kutangaza uzinduzi wa tamthilia hizo zilizokuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu.
Amebainisha kuwa tamthilia hizo zilizobeba simulizi za kuvutia si tu kwamba zinakuja kuleta mapinduzi ya tasnia ya tamthilia nchini, bali zinaakisi maisha halisi ya Watanzania wa rika zote na zinahusisha waigizaji wenye vipaji na viwango vya juu.
“Uzalishaji wa tamthilia hizi mbili Mtaa wa Kazamoyo na Lolita umezingatia mahitaji ya soko kwani umetumia vifaa vya uzalishaji vya kisasa na ubora wa hali ya juu wenye uwezo wa kutoa kazi katika viwango vya picha zenye ubora na angavu yaani HD (High Definition). Lengo letu la kufanya mambo yote haya ni kuendeleza dhamira yetu ya kutoa burudani ya hali ya juu kwa watazamaji wetu”Amesema Sophia Mgaza.
Amesisitiza
kuwa Mtaa wa Kazamoyo na Lolita zimesanifiwa kwa uangalifu mkubwa ili
kuwapa watazamaji aina mbalimbali za simulizi za hadithi zenye kulinda
maadili ya Kitanzania, kutoa elimu kwa jamii na zinazotazamika na
familia yote na kutimiza majukumu yote matatu ya msingi yaani
kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha jamii.
Tamthiliya ya Mtaa wa Kazamoyo na Lolita zimetayarishwa kwa ustadi mkubwa zikishirikisha waigizaji mahiri, waandishi wenye ujuzi na watayarishaji wazoefu na zinajumuisha viwango vya juu vya uzalishaji na mbinu za hali ya juu ili kuhakikisha utazamaji wa kuvutia kwa hadhira.
Ameongeza kuwa waanatarajia kuanza kupokea filamu hivi karibuni ambazo wanategemea kupata hadithi zenye utafiti wakutosha, uhalisia wa kitanzania na kugusa jamii ya kimataifa na hadithi zenye stori ndefu isiyopungua dakika 90 na yenye viwango vya juu vya kimataifa inayoweza kuchezwa kwenye majumba ya Sinema pamoja na bajeti yake.
Kwa upande wake, Muandaaji wa Tamthilia ya Mtaa wa Kazamoyo, Mahsein Awadhi (Dkt. Cheni) amesema tamthilia hiyo inasimulia hadithi inayohusu maisha ya uswahilini na matukio wanayopitia wakazi wa Mtaa wa Kazamoyo. Huu ni mtaa wenye sifa ya wanawake kukaa vibarazani na kupiga stori, porojo pamoja na umbea huku vijana wa mtaa huu wakichagua maisha ya kuwa vibaka ili kupata vipato kwa njia fupi na nyepesi kwao.
Katika Mtaa huu viongozi wa Serikali ya Mtaa wanashindwa kudhibiti vitendo hivyo na unaweza kusema wanafurahishwa na tabia za wakazi wake na ndio maana wanakuwa mstari wa mbele kutetea maovu yanayoendelea dhidi ya vyombo vya dola.
Katika Mtaa wa Kazamoyo si ajabu kukuta watu wazima wakijihusisha kimapenzi na vijana wadogo. Hii ni hadithi iliyojaa msisimko, migogoro na hadithi za kuvutia kuhusu maisha halisi ya uswahilini.
“Tamthilia hii imezalishwa na Kampuni ya Cheni Arts Creation Company Limited na baadhi ya wasanii mashuhuri walioshiriki katika tamthilia hii ni pamoja na Mahsein Awadhi (Dkt. Cheni), Amina Ahmed, Mwene Shina, Ester Darwesh, Elizabeth Chijumba, Queen Masanja, Hashim Kambi, Abdallah Mkumbila (Mzee Muhogo Mchungu), Pili Lway (Mama Nyamayao) Hajji Seif, Amini Samofi, Karim Mandonga na wasanii wengine wengi waliopo katika tasnia na wale wanaochipukia.” Amesema Dkt.Cheni.
Nae, Muandaaji wa Tamthilia ya Lolita, William Mtitu amesema tamthilia hiyo inatoa simulizi ya maisha ya vijana wa kisasa na namna wanavyokabiliana na changamoto za kimahusiano yaliyojaa usaliti. Tamthilia hii pia inatoa simulizi ya familia mbili zilizodhulumiana pesa na hivyo kila upande ukiapa kulipiza kisasi kwa mwenzake, lakini kabla kisasi hakijakamilika familia mojawapo inapata ajali ya ndege na kufariki dunia na hivyo kumwacha binti yao kipenzi katika malezi ya familia hasimu ya wazazi wake.
Familia hiyo inaamua kudhulumu mali zote zilizoachwa na wazazi wa binti huyu ambaye baadaye anakuja kupendana na mtoto wa kiume wa familia hii na siku ya harusi yao anapata ajali mbaya ya gari na hivyo kumsababishia ulemavu.
Ajali
hiyo imesababishwa na kijana aliyekuja kugundulika baadaye kuwa ni
ndugu yake wa damu. Baada ya ajali hii, siri nyingi zinaanza kugundulika
kuwa rafiki yake kipenzi ana uhusiano wa kimapenzi na mume wake, huku
mume wake naye akiwa na mpango wa kumdhulumu mali zote alizoachiwa na
baba yake. Kugundulika kwa siri hizi kunazua migogoro na hali ya
sintofahamu katika jamii inayowazunguka. Tamthilia hii imejengwa na
migogoro mingi ya kimapenzi baina ya marafiki, wazazi na vijana wadogo
na kati ya familia na familia. Ni simulizi ambayo unatakiwa kuiona
mwenyewe ili kuielewa vizuri.
“Tamthilia hii imeandaliwa na Magazijuto Pictures chini ya muandaaji William Mtitu. Miongoni mwa waigizaji mashuhuri katika tamthilia hii ni pamoja na Angel Mazanda, Mariam Ismail, Christopher Mziwanda, Romeo George, Genevieve Mpangala, Dennis David, Gysell Ngowi, Sadam Nawanda, Cojack Chilo, Careen Simba, Jacqueline Materu, Neema Malita, Khalid Kuraish na wasanii wengine wengi wanaofanya vizuri katika tasnia ya filamu Tanzania” Amesema Bw. Mtitu.
Hata hivyo tamthilia hizo zinachukua nafasi ya Fungu Langu itakayofikia tamati tarehe 29 Julai 2023 na Jeraha itakayofikia tamati tarehe 10 Agosti, 2023 ambapo Burudani zote hizo zinapatikana kwa malipo ya kifurushi cha Shilingi 8,000 kwa watumiaji wa kisimbuzi cha dishi na antena.
No comments:
Post a Comment