HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2023

DC MATINYI ATEMBELEA BANDARI KAVU TEMEKE AWAPA MATUMAINI WAMILIKI UCHUMI WAO KUKUA MARADUFU

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mobhare Matinyi  akizungumza  na wafanyakazi  wa ICD iliyopo eneo la Uwanja wa Taifa (hawapo pichani) mara  baada ya  kufanya ziara kwenye bandari  kavu, Dar es Salaam.

Mbunge wa Temeke Dorothy Kilave  akimsikiliza DC  wa Temeke alipokua akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa  HESU Investment Limited.


Na Khadija Kalili 


MKUU wa Wilaya ya Temeke,  Mheshimiwa Mobhare Matinyi, amesema kuwa mabadiliko ya bandari yatakayofanyika yatazinufaisha zaidi bandari kavu (Inland Container Depot - ICD) kuliko wanachopata sasa huku akiwaambia wasiwe na hofu endapo bandari ya Dar es Salaam itapata mwekezaji wa kuhudumia makasha.


Mheshimiwa  Matinyi amesema hayo Agosti 3  2023 Dar es Salaam baada ya kufanya ziara katika bandari kavu iliyoko chini ya kampuni ya HESU Investment Limited iliyopo Wilayani Temeke. 

Katika ziara hiyo aliambatana na ujumbe wa viongozi mbalimbali wa Temeke akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo Mheshimiwa Dorothy Kilave.


Mhe. Matinyi amesema kuwa alifanya ziara tofauti na kuzungumza na Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Selemani, ili kujua kuhusu mabadiliko yakayofanyika kwa wawekezaji wa Temeke  wanaomiliki  bandari kavu (Inland Container Depot - ICD).


“Niliuliza matokeo ya mabadiliko kwa sababu najua wawekezaji wakipata na wananchi wa Temeke watapata na serikali kuu na pia na Manispaa ya Temeke zitapata fedha za kufanyia shughuli za maendeleo kama kujenga shule na vituo vya afya,” amesema Mhe. Matinyi.


"Mkurugenzi wa Bandari  ya Dar es Salaam amenihakikishia kuwa hamtapoteza kitu zaidi ya kuimarika zaidi; hivyo jitayarisheni kutanua wigo wa utendaji wenu wa kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa  wananchi wa Temeke kwa sababu hii ni habari njema kwa wenye biashara ya ICDs. 


"Mnakwenda kupata zaidi ya mara dufu ya mnachopata sasa hivi, wenye biashara hiyo mtaongezeka au kupanua biashara zenu zaidi,” amesema DC Matinyi.


DC Matinyi ametumia  nafasi hiyo ya ziara yake  kujitambulisha ikiwa ni mwezi mmoja tangu ateuliwe na Mheshimiwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na asema atawatembelea wadau wa bandari waliopo Wilayani Temeke ili kuwahakikishia kwamba shehena inakwenda kuwa kubwa.


Mhe. Matinyi  amesema maamuzi ya Rais Dkt. Samia kununua mitambo mitatu ya kupakulia na kupakia makasha kila mmoja umegharimu shilingi bilioni 40 hadi 50 ndiyo sababu ya bandari hii kuvuka malengo yake hivi sasa.


Ameongeza  kwa kusema  kuwa kufikia mwaka 2030 inatarajiwa kuwa bandari ya Dar es Salaam itakuwa ikihudumia tani milioni 38 za shehena kutoka nchi jirani. 


Amezitaja nchi hizo kuwa ni Uganda, Congo, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Sudan Kusini, Comoro isiyokuwa na bandari kubwa na Msumbiji pia licha ya kuwa ina bandari zake. 


"Kwa sasa nchi hizi zina mizigo inayozidi tani milioni 70 lakini ni tani milioni 8.5 tu ndizo zilizohudumiwa na bandari ya Dar es Salaam kwa sababu mingine ilipitia bandari za Mombasa, Beira, Maputo, Durban na Walvis Bay", amesema Matinyi.


DC Matinyi amesema kuwa  wanajivunia kuona bandari hiyo ikifanya kazi na nchi karibu 11 ikiwemo mwenyeji Tanzania na kitendo hicho kinaongeza mapato ya serikali huku akitolea mfano mwaka wa fedha uliopita serikali iliipa bandari hiyo lengo la tani milioni 19.6 lakini ikafikisha tani milioni 21.27.


DC Matinyi amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakusanya asilimia 37 hadi 40 ya makusanyo yote kutoka bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni kodi na ushuru wa forodha na kwamba wawekezaji wakiongeza mizigo serikali inatarajia kiwango hicho kufikia asilimia 65 au zaidi.


“Bandari ya Dar es Salaam si kitu kidogo bali ni kitu kinachoweza kulipa taifa letu nguvu kubwa za kiuchumi katika eneo hili la Aftika,” amesema Matinyi.


Aidha DC Matinyi amesema kuwa endapo suala la mabadiliko ya bandari  litafanyika basi Kampuni hiyo ikumbuke  kutoa kipaumbele zaidi kwa vijana wa Temeke ikiwezekana kuwaajiri hata 2,000 badala ya 250 ilionao sasa.


Meneja wa Kampuni ya Hesu Investment Ltd, Hafidh Mana, amesema kuwa  Kampuni hiyo inafanya kazi na zaidi ya watu 600 ambapo kati ya hao wenye  ajira  za kudumu  ni 250.


Mh.Matinyi amemaliza kwa kusema zaidi kuwa Rais  Dkt. Samia anataka bandari hii iendelezwe zaidi kwa kuongeza magati namba 12 hadi 15 na kuboresha uendeshaji wa magati yaliyopo sasa.

No comments:

Post a Comment

Pages