Na John Marwa
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara NBC PL, Yanga SC inashuka dimbani kumenyana na watoza ushuru wa Kinondoni KMC FC katika Dimba la Azam Complex mchezo wa kwanza wa msimu huu kunako Ligi Kuu.
Yanga wanashuka dimbani leo wakihitaji kukusanya pointi tatu muhimu huku wakijua mtani wao Simba SC amekalia usukani wa Ligi baada ya kucheza michezo miwili nna kushinda yote.
Unatarajiwa kuwa mchezo wa aina yake kutokana na upinzani mkali ambao KMC wamekuwa wakiutoa wanapokutana na Miamba ya soka la Tanzania licha ya kupoteza michezo mingi dhidi yao.
Ni wazi mzani wa matokeo utaegemea kwa Yanga kuibuka na ushindi jioni ya leo licha ya kuwa KMC wana timu nzuri na benchi zuri la ufundi likiongozwa na Abdul Hamid Moallin ambaye amewahi kuinoa Azam FC.
Timu hizo kutoka Jiji la Dar es Salaam zimekutana mara 10 Yanga ikishinda mechi saba sawa na asilimia 70, huku sare zikitoka mara mbili sawa na asilimia 20 huku KMC wakishinda mchezo mmoja sawa na asilimia 10.
Yanga wao wanaanza msimu chini ya Kocha mpya Miguel Angel Gamondi ambaye amechukua mikoba ya Nasreddine Nabi ambaye aliachana na Mabingwa hao mara baada ya kuwapatia ubingwa wa Ligi, ASFC na Ngao ya Jamii pamoja na kuwafikisha Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika CAF CC.
Tayari msimu huu Yanga imepoteza Kombe moja kati ya hayo matatu ambayo walibeba msimu uliopita, sasa wanaianza safari ya kutetea NBC PL msimu huu.
Ni vita ya mjini Darslaam kati ya Ilala wanakotoka Yanga SC dhidi ya KMC FC ya Kinondoni ndani ya mahakama ya soka Azam Complex Chamazi ndani ya Temeke.
.jpg)


No comments:
Post a Comment