HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 04, 2023

SHIME: LAZIMA LIBAKI NYUMBANI

 Na Mwandishi Wetu


LAZIMA Kombe libaki nyumbani, Hii ni kauli ya kocha Mkuu wa timu ya Tanzania ya wasichana U-18, Bakari Shime kuelekea mchezo wa mwisho wa mashindano ya kuwania ubingwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA U18.


Kauli hiyo inakuja ikiwa ni mara baada ya Uganda kuwabugiza Burundi mabao 7-0, na Sasa Lazima Tanzania kushinda mchezo wao dhidi ya Uganda hapo kesho kwani wote wana pointi 9, kila timu ikishinda mechi zote tatu na sasa lazima mmoja ashinde ili kuwa Bingwa wa kwanza wa Makala ya kwanza ya mashindano hayo.


Timu hizo zinashuka kwenye dimba la Azam Complex  Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, leo majira ya saa 12:00 jioni, ukitanguliwa na mchezo kati ya Zanzibar dhidi ya Burundi ambao wote hawajashinda mchezo wowote.


Kocha Shime amesema utakuwa mchezo mgumu na ushindani mkubwa kwa sababu wote wana alama sawa na kila mmoja anahitaji ushindi katika mechi ya mwisho.


Amesema anaimani kuwa ana kikosi bora katika mashindano hayo lakini hawataidharau Uganda kwa sababu inawapa ushindani miaka yote kila wanapokutana.


“Mechi ni ngumu kwa sababu ya upinzani wetu lakini hatuhitaji kuona kombe linaondoka hapa kwetu, tunapambana kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo wetu huo na kutwaa ubingwa wa CECAFA U18. 


"Kama nilivyosema awali kuwa baada ya mechi na Zanzibar nina kibarua kingine kigumu dhidi ya Uganda ambapo kwetu ni fainali na tumejiandaa vizuri kushinda,” amesema Shime. 


Ameongeza kuwa anaimani na wachezaji wake kufanya vizuri baada ya kufanyia kazi mapungufu ya michezo iliyopita sasa wako tayari kwa ajili ya kutetea bendera ya Taifa kwa kuhakikisha kombe hilo linabaki katika ardhi yaTanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages