Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa Klabu ya Simba umesema kwa usajili walioufanya kuelekea msimu wa 2023/24 hawataacha kombe lolote kwenye michuano ya ndani na kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema malengo yao makubwa ni kufanya vizuri katika kila mashindano.
Amesema wanamatarajio hayo kwa sababu ya aina ya wachezaji waliowasajili watayakia malengo yao ya kutwaa mataji yote ya ndani na kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Tumefanya usajili mzuri, matumaini yetu msimu huu ni kuchukuwa mataji yote ya ndani lakini pia kufika hatua ya nusu fainali ya ligi ya Mabingwa Afrika," alisema Ahmed.
Ameongeza kuwa kwa hapa nyumbani hawaachi lolote wanachukuwa kila kilichopo mbele yao kwa sababu wanaimani ya kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.
Naye Mchambuzi wa video za mechi wa Klabu ya Simba, Kelvin Mavunga ametoa tahadhari kwa wapinzani wao kutokana na kikosi imara walichokuwa nacho kwa msimu mpya wa mashindano.
Amesema anaitamani Yanga hata kesho kwani wanayo maandalizi mazuri kuelekea msimu unaokuja wakiyataka makombe hapa nchini lakini pia kufanya vizuri Kimataifa.
Kauli ya mchambuzi huyo ni baada ya kuwafatilia Yanga katika kila kona na baada ya kuiona mechi yao ya kirafiki ya kimataifa waliyocheza siku yao ya wiki ya Mwananchi dhidi ya Kaizer Chiefs.
Amesema safari hii anaimani kubwa ya kuendelea na jukumu lake la kuwasoma wapinzani na kuwahakikishia wanasimba kuwa watawafunga sana wapinzani wao.
"Mechi iliyopita tuliwafunga, sasa tutaendelea kuwafunga sana maana raha yangu ni kuona tunawafunga Yanga, kokote tutakapokutana nao iwe ngao ya jamii au ligi tutawapiga tu," alisema Mavunga.
Aliongeza kuwa msimu huu wamekuwa na kikosi imara na bora kuliko misimu iliyopita na watafanya vizuri na kuhakikisha wanawanyima raha wapinzani katika ligi kuu na michuano ya kimataifa.
Kuelekea tamasha la Simba Day, uongozi wa klabu hiyo umemtangaza staa wa muziki wa kizazi kipya nchini, Ally Kiba ‘Alikiba’, ndiye mtumbuizaji mkuu katika tamasha la Simba ‘Simba Day’, litakalofanyika keshokutwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ikiwa ni makala ya 15 ya tamasha la Simba Day, imemtangaza Alikiba kwa kumsajili kama mwanachama mpya wa timu hiyo, ambaye awali alikuwa ni shabiki wa Yanga.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula, alisema waliangalia msanii ambaye anapendwa na watu wengi, wakaamua kumthamini kwa kumkaribisha katika klabu hiyo.
“Tunajua kuwa Ali Kiba ni msanii mkubwa Afrika, tunaamini kwa kufanya nae kazi atakuwa balozi mzuri wa klabu yetu katika mataifa mbalimbali ambayo anakwenda kufanya kazi,” amesema Kajula.
Ali Kiba anawashukuru Simba kwa kutambua thamani yake anaamini atakuwa na furaha akiwa hapo kutokana na rekodi nzuri walizonazo katika mashindano mbalimbali.
“Nimepata mapokezi makubwa Simba, moyo unapenda unapo thaminika. Kiukweli nilikuwa nawaonea wivu sana Wanasimba, asanteni kwa kunikaribisha, tutafurahi pamoja kwa kusikiliza nyimbo nzuri, nimeingia katika klabu hii kwa zawadi ya ngoma kali itakuwa mitandaoni hivi karibuni inaitwa ‘Mnyama’, siku ya Simba mjae uwanjani kwa wingi kuburudika pamoja,” amesema nyota huyo.
No comments:
Post a Comment