HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 05, 2023

TANZANIA MABINGWA WA CECAFA U18

 Na John Marwa


Timu ya Taifa ya Tanzania Wasichana U-18 imetwaa ubingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati CECAFA baada ya kuwatungu Uganda U18 bao (1-0).


Mchezo huo wa kukata na shoka umemalizika usiku huu Uwanja wa Azam Complex, ambapo ulikuwa mchezo wa mwisho wa mashindano.


Kabla ya mchezo wa leo Tanzania na Uganda walikuwa na pointi sawa kila timu ikishinda mechi tatu za awali na kujikusanyia pointi 9 lakini Uganda wakiongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.


Tanzania iliingia kutafuta ushindi pekee Ili kuwa Mabingwa wakati Uganda wao walihitaji  kushinda ama sare ili kuwa Mabingwa.


Kipindi cha kwanza Tanzania ilianza kwa kuhanikiza mashambulizi langoni mwa Uganda huku Uganda wao walicheza kwa kujilinda kwanza na  kushambulia kwa kushitukiza.


Dakika 15 za mwisho kuelekea mapumziko Tanzania walipiga kambi langoni mwa Uganda na kupelekea kupata mpira wa adhabu ambayo ilileta kizazaa na Winifrida Gerald kuachia shuti kali dakika ya 41 na kuipatia Tanzania bao hilo la kuongoza na la ushindi.


Kipindi cha pili Uganda walirejea kwa kwa kasi, wakishambulia kupitia kwenye mapana ya Uwanja lakini haikuweza kuzaa matunda kwani Tanzania waliziba mianya yote huku walicheza nyuma ya mpira muda mwingi.


Hadi dakika 90 zinatamatika Tanzania bao (1-0) Uganda. Matokeo hayo yameifanya Tanzania kufikisha pointi 12 huku Uganda U18 wakisaliwa na pointi 9 ambazo zimewaweka nafasi ya pili.


Ethiopia wao wameshika nafasi ya tatu na pointi zao 6. Burundi wameshika nafasi ya nne na pointi zao 3, huku Zanzibar wakibuluza mkia bila kuonja ushindi katika mashindano hayo.


No comments:

Post a Comment

Pages