Je Unajua Ukipiga Mswaki Hutakiwi Kusukutua? Dr. Nasriya Ali, Anaelezea Jinsi ya Kupiga Mswaki Sahihi kwa Afya Bora ya Kinywa na Meno.
Unapofikiria kuhusu utunzaji wa afya ya kinywa, moja ya mazoea ya kila
siku ambayo usipopiga kwa usahihi yanaweza kuathiri afya ya kinywa na
meno .Lakini je, unajua kwamba kuna njia sahihi ya kufanya hivyo ili
kuhakikisha afya bora ya kinywa na meno?
Kupiga mswaki ni hatua muhimu katika kudumisha afya ya kinywa na meno.
Lakini mara nyingi, watu hufanya makosa yanayoweza kusababisha matatizo
ya kinywa na meno. Dr. Nasriya Ali kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
Temeke anasema, "Moja ya makosa yanayofanyika ni suala la kusukutua
baada ya kupiga mswaki. Kusukutua kunasababisha kuondoka kwa madini
yaliyopo katika dawa ya mswaki ambayo yalitakiwa kubaki kwa ajili ya
kulinda meno.
Dr. Nasriya Ali anashauri njia sahihi ya upigaji mswaki na vitu vya
kuzingatia wakati wa kupiga mswaki.
Hivyo basi Kabla hujaanza kupiga
mswaki kuna vitu unatakiwa kuvizingatia Tumia Mswaki mzuri
Mswaki
mzuri ni ule wenye nyuzi au brashi laini, kulingana na umri wa
mtumiaji. kuna miswaki ya watoto na ya watu wazima. Kutumia Mswaki wa
aina hii utawezesha kufikia maeneo yote ya meno bila kusababisha madhara
katika meno na fizi.
*Kuzingatia aina ya dawa*
unaweza kutumia dawa ya aina yoyote lakini dawa inapaswa kuwa na madini
ya floride madini ya floride ni madini yanayozuia meno kutoboka na
kufanya meno kuwa imara, na ndio maana unapo maliza kupiga mswaki
hupaswi kusukutua na maji, unatakiwa kuacha hivyo hivyo ili kuruhusu
madini yaliyopo katika dawa ya mswaki kufanya kazi yake katika kinywa
chako.
*Kupiga mswaki kwa usahihi au kutumia njia sahihi ya kupiga mswaki*
njia sahihi ni kama ifuatavyo, utachukua mswaki wako na kuweka dawa ya
meno yenye madini ya floride utaanza kupiga kwa taya moja moja kwa
kupindisha mswaki wako kidogo kuelekea kulia ama kushoto, utaanza kupiga
mswaki kwa mwendo wa kuzungusha taratibu ili kuwezesha mswaki kuingia
katikati ya meno na kuepusha kuumiza fizi. Meno ya mbele juu unatakiwa
kusimamisha mswaki na kusafisha. Utasafisha pia maeneo ya nyuma ya meno
yanayohusika na utafunaji na utafanya hivyo hivyo kwa taya nyengine ni
na kumalizia kwa kusugua ulimi kwa taratibu.
*Muda unaotumia kupiga mswaki*
Unatakiwa Kupiga mswaki kwa dakika zisizopungua dakika mbili, Unatakiwa
kupiga mswaki mara mbili kwa siku yaani baada ya kunywa chai asubuhi ili
kuzuia mabaki ya chakula yasiwepo kwenye kinywa muda mrefu na wakati wa
kwenda kulala na kabla ya kulala unapaswa kupiga mswaki.
Dr. Nasriya Ali anasisitiza umuhimu wa kutembelea daktari wa meno kwa
ukaguzi na uchunguzi wa kawaida angalau mara mbili kwa mwaka. Anasema,
"Uchunguzi wa kinywa na meno unaweza kugundua mapema matatizo yoyote na
kuchukua hatua za haraka." Na katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke
kuna madaktari bingwa na vifaa vinavyowezesha utoaji huduma sahihi wa
kinywa na meno ambao watu wengi wanaweza wakapuuzia matatizo walionayo.
Kwa kumalizia, Dr.Nasria Ali anasema, "Upigaji mswaki ni mazoea rahisi
lakini muhimu kwa afya ya kinywa na mwili kwa ujumla. Kwa kufuata njia
sahihi na kujali afya yako ya kinywa, unaweza kuhakikisha una kinywa
kizuri na chenye afya kwa maisha yako yote."
Kuwa na kinywa chenye afya ni muhimu sana kwa afya ya jumla. Kwa
kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa kinywa na meno, unaweza kuboresha afya
yako ya kinywa na kufurahia maisha bora zaidi. Makala hii imeandikwa na Cleopatra Mokiwa.
No comments:
Post a Comment