Serikali kuwapa ushirikiano wawekezaji
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo cha kwanza cha kisasa cha kujazia gesi asilia kwenye magari na karakana ya kuweka mfumo wa gesi asilia ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa mipango ya Serikali kuchochea matumizi ya gesi asilia kama nishati safi na salama kwa mazingira jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko leo amezindua kituo cha kwanza cha kisasa cha kujazia gesi asilia
kwenye magari na karakana ya kuweka mfumo wa gesi asilia ikiwa ni
muendelezo wa utekelezaji wa mipango ya Serikali kuchochea matumizi ya
gesi asilia kama nishati safi na salama kwa mazingira.
Uzinduzi
huo umefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 11 Novemba, 2023 na
kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Balozi Sherif
Ismail wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Balozi Isaac Njenga wa Jamhuri ya
Kenya, Balozi Fred Mwesigye wa Jamhuri ya Uganda, Mha. Felchesmi
Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Mtendaji Mkuu wa kampuni ya
TAQA, Pakin Kafafy.
Dkt.
Biteko amesema kuwa, kujengwa kwa kituo hicho na TAQA Arabia na
washirika wao JCG Oil & Gas niutekelezaji wa maono ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye
amekuwa na maono ya kuleta wawekezaji nchini wakiwemo wanaowekeza kwenye
Sekta ya Nishati, hivyo ameahidi kuwa Wizara itafanyia maelekezo yake
ili kutekeleza maono yake.
Dkt.
Biteko amesema kuwa, Serikali inaweka msukumo mkubwa kwenye matumizi ya
gesi ya asilia yakiwemo magari, mitambo ya viwandani, hivyo kuzinduliwa
kwa kituo hicho ni kuonesha azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa Gesi
inayopatikana Tanzania inatumika ndani ya nchi kwanza.
Amesema
kituo hicho kitajaza gesi kwenye magari 800 kwa siku na kina pampu sita
zitakazojaza gesi kwenye magari sita kwa maramoja ambapo ujazaji wa
gari moja utakuwa ni wa dakika tatu hivyo hicho ni kituo kikubwa
kitakachosaidia kubadilisha magari na kufanya yatumie gesi badala ya
mafuta pekee.
Amesema
Kampuni hiyo inatarajia kujenga vituo 12 vya CNG jijini Dar es Salaam
ili kuwa na vituo vingi zaidi vya kujazia gesi kwenye magari.
Ameongeza
kuwa, kampuni hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) wapo kwenye majadiliano ili kujenga vituo vidogo vya
Gesi ya Kusindika (LNG) ili kuweza kutoa Gesi jijini Dar es Salaam na
kupeleka kwenye mikoa mbalimbali ili nayo iweze kujaza gesi hiyo kwenye
magari..
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika uwekezaji wao ili kuchochea ukuaji wa nishati nchini.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo ameishukuru
Wizara ya Nishati kwa kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya usambazaji nishati katika maeneo
yote ikiwemo gesi asilia.
Amesema
kuwa Wilaya ya Ilala, inaona faraja kufunguliwa kwa kituo wilayani humo
kutokana na kuwa kitovu cha Mkoa wa Dar es Salaam kwani Wilaya hiyo ina
wananchi wasiopungua milioni 1.6 ukilinganisha na idadi yote ya wakazi
wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao jumla yao ni milioni 5.3.
No comments:
Post a Comment