Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS imesema kwa kipindi cha Mwaka mmoja, ukubwa wa mifuko umeongezeka kutoka Sh. Bilioni 996.5 Juni 30, 2022 hadi kufikia Sh trilioni 1.535 Juni 30, 2023.
Hayo yamesemwa jijini humo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UTT AMIS Simon Migangala akizungumza na wanahabari kuhusu Mikutano ya Mwaka ya Mifuko ya Umoja, Wekeza Maisha, Watoto, Kujikimu, Ukwasi na Hatifungani inayofanyika kuanzia leo Novemba 18 hadi 20 jijini Dar es Salaam.“Ongezeko hili la kiasi cha shilingi bilioni 538.9 ni sawa na asilimia 54.0 ikilinganishwa na ongezeko la shilingi bilioni 383.7. Ongezeko hili la ukubwa wa Mifuko linatokana na imani ya wawekezaji kwetu, elimu itolewayo juu ya akiba na uwekezaji pamoja na akiba shindani kwenye Mifuko,” amesema Migangala.
Migangala ameeleza kuwa Utendaji wa Mifuko kwa kipindi hicho umeendelea kuwa mzuri kwamba faida kwa wawekezaji ilikuwa kubwa ikilinganishwa na vigezo linganifu.
Amebainisha
kuwa faida kwa mwaka kwa upande wa Mifuko inayowekeza kwenye hisa na
maeneo yenye Mapato ya kudumu kuwa ni pamoja na Mfuko wa Umoja asilimia
11.2, Mfuko wa Wekeza Maisha asilimia 12.5, Mfuko wa Watoto asilimia
12.4.
Mifuko mingine ni Mfuko wa Jikimu asilimia 14.0 ikilinganishwa na asilimia 7.6 ya kigezo linganifu huku akibainisha kuwa kwa Mifuko iliyosalia yenye uwekezaji kwenye maeneo yenye Mapato ya kudumu faida kwa Mfuko wa Ukwasi ni asilimia 12.5 na Mfuko wa Hatifungani ni asilimia 12.3 ikilinganishwa na asilimia 9.7 ya kigezo linganifu.
Kuhusu maendeleo ya Soko la Hisa, amesema Utendaji wa Kampuni za ndani ya Nchi unapimwa kwa kuangalia mabadiliko ya Fahirisi (Tanzania Share Index).
Hivyo Migangala, ameeleza kuwa katika mwaka wa Fedha ulioishia Juni 30, 2023, Fahirisi imeonesha kuwa na ongezeko la asilimia 4.1 kutoka 3,928.5 kwa Juni 30, 2022 hadi 4,091.8 kwa Juni 30, 2023.
Amesema hiyo inamanisha kuwa katika kipindi cha Mwaka ulioishia Juni 2023, bei za Hisa kwa Kampuni za ndani ya Nchi ziliongezeka sawa na asilimia 4.1.
Amezitaja sababu zilizosababisha kupanda kwa bei za Hisa kuwa ni pamoja na Utendaji mzuri wa Kampuni za ndani kwenye soko la Hisa la Dar es Salaam, kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa Ndani na nje na uboreshwaji wa mazingira ya uwekezaji hapa nchini.
Katika mpango mkakati wa miaka mitano utakaoishia mwezi Juni 2024, amesema Kampuni imeazimia kujikita kwenye matumizi ya Teknolojia katika kutoa huduma KWA wawekezaji.
Kwa upande wake, Mwenyeki wa Bodi ya UTT AMIS, Casmir Kyuki amewaalika wawekezaji wa Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS kuhudhuria Mikutano hiyo inayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.Amesema Mikutano hiyo hufanyika ili kukidhi matakwa ya Kanuni ya Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya Mwaka 1997.
No comments:
Post a Comment