HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 14, 2024

Bandari ya Dar es Salaam yavuka malengo kuhudumia Shehena, Idadi ya Meli kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2023

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema Bandari ya Dar es Salaam imevuka malengo ya kuhudumia Shehena, idadi ya meli na ukubwa wa meli katika kipindi cha Julia hadi Desemba 2023.



Hayo yamebainishwa jijini humo na Mkurugenzi Mkuu wa TPA Plasduce Mbossa akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu utendaji na uendeshaji wa Bandari nchini.


Amesema katika kipindi hicho Bandari ya Dar es Salaam  imefanikiwa kufanya huduma zaidi ya malengo yake ambapo imehudumia takribani meli 979 kati ya meli 792 zilizokuwa zimekusudiwa.


Amesisitiza kuwa katika kipindi hicho bandari imehudumia abiria takribani milioni 1 kati ya 900,000, makasha 990,000 kati ya lengo la kuhudumia makasha 500,000, huku mizigo ikiwa ni tani milioni 17.2 kati ya tani milioni 15.6 zilizokusudiwaa.


Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo ameongeza kuwa, kutokana na maboresho ya bandari meli hadi 12 zinahudumiwa kwa wakati mmoja, hivyo kupelekea wastani wa meli 100 kuhudumiwa kwa mwezi mmoja, kutoka meli 70 ndani ya mwezi mmoja. 


Ameeleza kuwa, kutokana na mikakati mbalimbali ya serikali ya kukuza uchumi wa nchi kumepelekea kuwepo kwa ujenzi wa miradi mbalimbali na hivyo kuongezeka kwa kiwango kikubwa cha mizigo inayopita katika bandari hiyo.


Akizungumza kuhusu Bandari ya Bagamoyo  Mbosa amesema "Tumeona haja ya kuharakisha ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kutokana na hali iliyopo, kwamba baadhi ya meli haziwezi kuhudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kutokana na magati kuwa mdogo,"


Hata hivyo, Mbossa amesema wanatarajia mradi huo kukamilika mwaka 2028 na kwa sasa mchakato wa kumpata mzabuni unaendelea.

No comments:

Post a Comment

Pages