NA MAGENDELA HAMISI
CHUO cha Elimu ya Ufundi Stadi cha Elimu Furahika cha Buguruni Malapa kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, kimeanzisha kozi mpya kwa vijana wasiojua kusoma na kuandika kwa lengo la kutimiza ndoto zao kupitia elimu.
Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. David Msuya amebainisha hayo leo Januari 5,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amefafanua kwa kozi hiyo wanapokea vijana kuanzia miaka 14 hadi 30.
“Kozi hiyo itaanza Februari mwaka huu kwa muda wa mchana na itatolewa bure watakacholipia ni fomu ya usajili tu, hivyo tunawakaribisha wasichana kwa wavulana wasiojua kusoma na kuandika wajitokeza kwa wingi kujisajili wingi ili tuanze masomo kulingana na ratiba.
“Hapa watafundishwa kuanzia hatua ya darasa la kwanza hadi la tano na tunaamini kwa muda huo watakuwa wanajua kusoma na kuandika vizuri na kuweza kuperuzi katika mitandao ya kijamii kupitia simu yake na kufahamu ulimwengu namna unavyokwenda bila tatizo,” amesema.
Ameongeza kuwa wameamua kuanzisha kozi hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa kundi la vijana wasiojua kusoma na kuandika hivyo wakifundishwa watakuwa wamewaondoa katika giza zito katika maisha yao ya kila siku.
Amefafanua kuwa vijana walio katika kundi hilo wasione aibu kujiunga na Chuo cha Furahika kwa ajili ya kujifunza kusoma na kuandika kutokana na kwamba wapo wamefika hapo kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kufiwa na wazazi na kutopata mtu wa kumpeleka shule kwa wakati sahihi.
Pia kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii wanajipanga kutoa elimu ya malezi kwa walimu wa shule ya awali na jamii ili waweze kutoa huduma bora kwa watoto wanaojiunga kwenye shule zao.
Dkt. Msuya amefafanua kuwa elimu hiyo ambayo wanaitoa bure itakuwa ni moja ya fursa kwa watakaohitimu, kupata ajira kwenye shule mbalimbali nchini za awali .
Kati hatua nyingine, Dkt Msuya amesema mkakati wao mwingine ni kufundisha wafanyakazi wa kazi za majumbani ili kuwapa uelewa mkubwa kuhusu namna ya kuhudumia familia na nyumba kwa ujumla.
“Wapo baadhi ya wafanyakazi wa ndani wanafanya kazi kwa mazoea huku wakiwa hawana ujuzi kitu ambacho wakati mwingine wanajikuta wakifanya ukatili kwa watoto pasipo kujua na kuingia kwenye matatizo, hivyo wakija kwetu tatizo la ukatili litaondoka ama kupungua kwa asilimia kubwa,” amesema.
Pia ametoa ushauri kwa akina dada wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, ikiwemo, Omani kabla ya kwenda huko wajiunge na Chuo cha Furahika ili kupata elimu na mafunzo sahihi namna ya kuhudumia nyumba na familia kwa ujumla ili kuondoa changamoto mbalimbali katika majukumu yao wanapokuwa ughaibuni.
No comments:
Post a Comment