WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii kuwa iendelee kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto kwani vinasababisha watoto wengi kukimbia familia zao na kukosa makao maalum.
“Jamii na Watanzania kwa ujumla kila mmoja ashiriki katika kulinda haki na ustawi wa watoto wetu. Hii ni nguvukazi ya Taifa letu hivyo basi, ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu letu sote. Mamlaka zinazohusika ziendelee kusimamia, kufuatilia na kuratibu vyema huduma za Makao ya Watoto zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali. “
Ameyasema hayo leo Ijumaa, Januari 5, 2024, wakati wa hafla ya chakula cha mchana na watoto wanaolelewa katika makao ya kulelea watoto ya SWACCO yaliyoko Manispaa Songea mkoani Ruvuma, ambapo amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii watekeleze kikamilifu wajibu wao ikiwemo kutambua vituo au makao na kutatua changamoto za ustawi zinazoikabili jamii na kutoa msaada wa kisaikolojia na afya ya akili kwa walengwa.
Pia, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe wanaweka utaratibu wa kuwatembelea wadau wanaoshirikiana na Serikali kutoa huduma kwa wenye uhitaji ili kutambua changamoto walizo nazo na kuzitafutia ufumbuzi, pamoja na kuwapa uelewa wa mipango na mikakati ya Serikali kuhusu huduma za ustawi wa jamii.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameitaka wizara inayohusika na masuala ya ustawi wa jamii iendelee kushirikiana na wadau kuongeza kasi ya utoaji elimu ya malezi chanya kwa wazazi/walezi na jamii kwa ujumla ili kuwa na nguvu kazi yenye tija kwa Taifa. “Nawashukuru wadau na wafadhili kwa kusimamia Makao haya ili kuhakikisha watoto wetu wanapata huduma stahiki za malezi na mahitaji muhimu. “
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania wote wahakikishe kuwa watoto wote wenye ulemavu wanapewa fursa ya kupata huduma za jamii ikiwemo elimu na waache tabia za kuwaficha ndani badala yake washirikishe mamlaka ikiwemo viongozi wa Mitaa, Vijiji, Kata na Wilaya ili kupata msaada.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa suala la kuwahudumia watu wenye ulemavu, kuwapatia vifaa saidizi pamoja na kuhakikisha kuwa wanaguswa moja kwa moja na maendeleo jumuishi, mafanikio yake hayamo katika mikono ya Serikali pekee, hivyo, ni muhimu kwa wadau wote kufanya kazi pamoja ili kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kupata fursa na kuishi bila utegemezi.
Kwa upande wake, Meneja wa kituo hicho Bw. John Chinguku amesema kituo hicho kilianzishwa Septemba 29, 2000 na Bibi Regina Chinguku akiwa na lengo la kusaidia na kuunga mkono jitihada za Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kupunguza changamoto za watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kwa kuwapatia huduma za afya, elimu, chakula, mavazi na makazi.
Meneja huyo alisema kituo kilianza kutoa malezi kwa watoto yatima wanne ambao aliwalea kwa kushirikiana na akina mama wengine ambao walikuwa wakijishughulisha na kilimo pamoja na kazi zingine za mikono kwa lengo la kupata mahitaji ya kila siku ya kuwahudumia watoto hao. Kwa sasa kituo kina watoto 50.
Naye, Bibi Anna Mugenya ambaye ni msaidizi wa Mkurugenzi wa kituo hicho ameishukuru Serikali kwa ushirikiano unaoutoa katika kituo na hivyo kurahisisha shughuli za uendeshaji yakiwemo malezi kwa watoto. Pia alimshukuru Waziri Mkuu kwa msaada wa vyerehani, vyakula na vifaa vya michezo ya watoto zikiwemo jezi na mipira ambavyo alivikabidhi leo kituoni hapo.
No comments:
Post a Comment