HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 07, 2024

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- AWEKA JIWE LA MSINGI SKULI YA SEKONDARI YA KONDE- PEMBA

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya selimu ili kuendana na fikara na falsafa za waasisi wa mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya kuwapatia elimu bure kwenye mazingira mazuri wananchi wake bila ya ubaguzi wa aina yoyote.


Hayo yamesemwa na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akiweka Jiwe la Msingi katika Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Amesema kuwa shabaha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kutatua changamoto ya nafasi katika skuli zetu za Maandalizi, Msingi na Sekondari ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia watoto kutembea masafa marefu ya kutafuta huduma ya elimu kwa kuondosha utaratibu wa wanafunzi kuingia katika mikondo miwili ya asubuhi na jioni.

 

Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga na kuimarisha Vyuo vya Mafunzo ya Amali kila Wilaya ili kutoa fursa kwa vijana ambao watakosa sifa ya kuendelea na masomo waweze kujiunga katika vyuo hivyo ambapo kwa sasa serikali imo katika mchakato wa ujenzi wa vyuo vya Amali vitano (5)  ambavyo vitawasaidia wananchi kuweza kujiajiri pindi watakapo maliza masomo yao.

 

Aidha Serikali inazidi kuwawekea mazingira bora wanafunzi wanaoendelea na masomo ya elimu ya juu kwa kuongeza bajeti kutoka shilingi za Kitanzania Bilioni 19.53 kwa mwaka 2020/2023 hadi kufikia Bilioni 29.5 kwa mwaka 2020/2024 sambamba na kuongezewa posho ya kujikimu kutoka shilingi laki moja na thelathini hadi kufikia laki moja na hamsini kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya Zanzibar na laki moja na themanini kwa wanafunzi wanaosoma vyuo vya Tanzania Bara ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kujiunga na Vyuo Vikuu.

 

Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais amewataka wananchi kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na serikali ya kuleta maendeleo, pamoja na kuwataka wanafunzi kuitumia fursa waliyonayo mashuleni kujipatia elimu pamoja na kuepuka vitendo vya viovu ikiwemo uvutaji wa bangi, wizi na ubaradhuli kwani yote hayo hayana mustakbali mwema wa maisha yao.

 

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Ali Abdulghulam Hussein amesema Rais wa Zanzibari na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussen Ali Mwinyi ameboresha maslahi ya walimu kwa kuwaongezea mishahara sambamba na kuwaajiri walimu zaidi ya (2000) lengo ikiwa ni kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika katika ufundishaji na usimamizi wa wanafunzi ili kupata matokeo mazuri yatakayotoa wataalamu wazuri watakaoitumikia nchi yao na Taifa kwa Ujumla.

 

Ghulam amesema wananchi wanapaswa kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo ni mkombozi wa Wazanzibari wanyonge waliotawaliwa na kunyanyaswa na  wakoloni waliowanyima nafasi ya kupata haki yao ya elimu

 

Amewataka walimu, wanafunzi na wananchi kuwakemea vikali wale wote wanaoyadharau na kuyabeza Mapinduzi na badala yake wawe mstari wa mbele katika kuelimishana juu ya umuhimu wa Mapinduzi kwa kizazi kijacho.

 

Akisoma Taarifa ya kitaalamu juu ya ujenzi wa mradi wa Skuli ya Konde Sekondari, Naibu Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanakhamis Adam amesema kukamilika kwa ujenzi wa skuli hiyo kutatoa nafasi kwa wanafunzi kuingia skuli kwa mwongo mmoja tu wa asubuhi na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani ambapo kila darasa litachukua wastani wa wanafunzi 45 tu.

 

Dkt. Mwanahamis amefahamisha kuwa ujenzi huo wa Skuli ya gorofa tatu(3) utakaokidhi mahitaji yote ya kusomea na kusomeshea hadi kumalizika kwake utagharimu zaidi ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 6.2 ambapo wanafunzi 1845 watapata nafasi ya kusoma skulini hapo.

 

No comments:

Post a Comment

Pages