WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wanapata haki ya kikatiba ya kupata habari kama ilivyoainishwa katika ibara 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Majaliwa amenukuu sehemu ya katika inayozungumzia haki ya wananchi kupata habari “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”.
Ameyasema hayo leo Jumamosi, Januari 6, 2024, wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa baada ya kuzindua studio za Redio Jamii- Ruangwa katika ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Lindi.
Amesema huduma bora za mawasiliano ni muhimu kwa kuwa ni kichocheo katika kuleta maendeleo ya jamii na nchi nzima kwa ujumla.
Mheshimiwa Majaliwa amesema ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025; Ibara ya 125 (a) imeielekeza Serikali kuendelea kutekeleza Sheria ya Huduma za Habari na. 12 ya Mwaka 2016 ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa wakati.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa uzinduzi wa kituo hiko ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya Ilani ambayo imedhamiria kuhakikisha kuwa sekta ya habari inaboreshwa ili kuwaongezea wananchi fursa ya kupata habari kwa kuongeza wigo wa upashanaji wa habari.
“Ni ukweli usiopingika kuwa huduma bora za mawasiliano ni muhimu sana kwani ni kichocheo cha kuleta maendeleo katika jamii yetu na nchi nzima kwa ujumla. Umuhimu huo unadhirika kutokana na mchango wake katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na pia katika masuala ya ulinzi na usalama. “
Waziri Mkuu amesema huduma ya mawasiliano ni chachu ya ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi, kwa kupitia mawasiliano taarifa mbalimbali muhimu za Serikali na sekta binafsi zinawafikia walengwa wote wakiwemo wananchi kwa wakati na kwa ufanisi na hatimaye kuleta tija inayokusudiwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa Redio Jamii- Ruangwa wahakikishe wanatunza na kutumia kwa uangalifu vifaa vilivyonunuliwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu na pia wasikilizaji waendelee kunufaika na huduma za utangazaji za Redio hiyo. "Vyombo vyote vya Habari zikiwemo redio na luninga fanyeni utafiti kabla ya kufikisha habari kwa wasikilizaji na watazamaji. "
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesetoa wito kwa watumishi wa redio hiyo wahakikishe wanakwenda hadi vijijini kwa ajili ya kuandaa vipindi mbalimbali vya maendeleo ya wananchi.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema vifaa vilivyofungwa katika studo hizo ni vya kisasa na vina uwezo wa kufika kilomita 200 kwa pande zote. "Redio hiyo inasikika katika wilaya za Liwale, Nachingwea, Kilwa na Masasi. "
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wialaya ya Ruangwa, Bw. Frank Chonya alisema dhamira ya redio hiyo ni kuwaelimisha, kuwaburudisha Wana-Ruangwa, hivyo aliishukuru Serikali kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 550 kwa ajili ya uboreshaji wa redio hiyo.
No comments:
Post a Comment