Baadhi ya wafanyabiashara wakiwa na furaha baada ya kupokea mfano wa hundi ya Sh. Mil. 270 kutoka Benki ya NMB kama malipo ya fidia ya mikopo baada ya kutokea maporomoko ya matope Disemba 3, 2023 Katesh, Hanang mkoani Manyara. (Na Mpiga Picha Wetu).Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja (wa tatu kulia), akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh. Mil. 270 mfanyabiashara Happiness Mlay (kushoto) zilizotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya kulipa fidia wateja 18 waliokuwa na mikopo ya biashara baada ya kutokea maporomoko ya matope Disemba 3, 2023 Katesh, Hanang mkoani Manyara, wa pili kulia ni Kamishna wa Bima, Dk. Baghayo Saqware na wa tatu kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Bima NMB, Martin Massawe. (Na Mpiga Picha Wetu).
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja (katikati), akipokea mfano wa hundi ya Sh. Mil. 270 kutoka kwa Kamishna wa Bima Dk. Baghayo Saqware (wa pili kushoto), zilizotolewa
na Benki ya NMB kwa ajili ya kulipa fidia wateja 18 waliokuwa na mikopo baada ya kutokea maporomoko ya matope Disemba 3, 2023 Katesh,
wilayani Hanang mkoani Manyara. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Bima wa
Benki ya NMB, Martin Massawe na wa tatu kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu
wa Kampuni ya Bima ya Reliance Tanzania, Ravi Shankar. (Na Mpiga Picha
Wetu).
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB imesaidia wajasiriamali wadogo na wakati walioathirika na maporomoko ya tope wilayani Hanang kulipwa fidia ya hasara walizopata kutokana na janga hilo lililotokea mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka jana.
Wahanga hao 18 wanaolipwa TZS milioni 270 na kampuni ya Reliance Insurance walikuwa na mikopo yenye kinga ya bima ya mshirika huyo wa NMB katika biashara ya huduma za bima zinazotolewa na benki (bancassurance) hiyo.
Kulipwa kwa wakati kwa wateja hao wa NMB ni matokeo ya kushiriki kikamilifu kwa taasisi hiyo katika kuyachakata malipo ya madai yao. Ulipaji wake ulitangazwa rasmi katikati mwa wiki jana katika Stendi ya Mabasi ya Katesh wakati wa hafla ya kukabidhi mfano wa hundi wa kiasi cha fidia hiyo.
Wazungumzaji kwenye shughuli hiyo hawakusisitiza tu umuhimu wa kukata bima bali pia walitoa wito wa kuongeza elimu kuhusu huduma hiyo hasa miongoni mwa wananchi wa kawaida ambao ufahamu wao wa masuala na faida za bima bado ni mdogo sana.
Akipambanua umuhimu wa bima katika maisha na usalama wa mali, Mkuu wa Idara ya Bima ya NMB, Bw Martine Massawe, alisema nafuu ya hasara waliyopata wahanga hao wa mafuriko ya Hanang ni kwa sababu yakuwa na kinga ya bima katika biashara.
Bw Massawe alisisitiza kuwa bima ni huduma inayosaidia kuzikabili hatari za kibiashara ambayo wajasiriamali wanapaswa kuhakikisha wanayo ili kijilinda hasa kifedha. Aidha, alisema bima inawasaidia pia kuzirejesha shughuli zao katika hali ya kawaida baada ya kuathirika na majanga kama maafa ya Hanang.
"Wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo ukabiliwa na changamoto nyingi na matukio yasiyotarajiwa hivyo kutokuwa na uhakika wa usalama uendelevu wa shughuli zao. Kwa mantiki hiyo, bima ni kitu muhimu kwa ajili ya kutoa ahueni kwa wahanga wa athari kama hizo ambazo uhatarisha maisha na mafanikio yao,” alibainisha.
Akisisitiza dhamira ya NMB kuchochea ukuaji wa matumizi ya bima nchini, afisa huyo alisema huduma hiyo haitoi tu usalama wa kifedha bali pia uwahakikishia wajasiriamali amani katika kutekeleza majukumu yao.
Kwa mujibu wa Bw Massawe, ushiriki wa NMB katika bima kunalenga hasa kusaidia ustawi wa biashara za ndani kupitia masuluhisho bunifu na pia kuchangia ukuaji wa sekta hiyo nchini.
Ili kutimiza malengo hayo, amewaomba wakazi wa Mkoa wa Manyara na Watanzania wote kwa ujumla kuzitumia bima mbalimbali zinazotolewa na kuzidi kubuniwa na benki hiyo.
"Benki yetu inazo bidhaa mbalimbali bora za bima ambazo ni mahususi kwa ajili ya kada mbalimbali za wananchi kimapato ambazo bei zake ni nafuu ikiwemo huduma ambayo malipo yake kwa mwaka ni TZS 10,000. Uzuri ni kwamba taratibu za upatikanaji wake zimerahisishwa ili kuwavutia watu wengi,” Bw Massawe alisisitiza.
Aidha, alibainisha kuwa mwaka huu benki hiyo itaendeleza kampeni ya Umebima ili kuzidi kuhamasisha matumizi chanya ya bima itakayoenda sambamba na utoaji wa elimu nchi nzima kuhusu umuhimu wa huduma hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Bi Janeth Mayanja alisema elimu hiyo inahitajika sana wilayani humo kutokana na watu wengi kuwa na uelewa mdogo wa huduma za bima na jinsi ya kuzipata.
Aidha, alisema utafiti wa awali wa kubainisha ukubwa wa janga lililowapata si tu ulibaini kuathirika kwa mamia ya wajasiriamali bali pia uligundua wengi hawakuwa na bima wala ufahamu wa faida zake.
“Kimsingi kiwango cha elimu kuhusu huduma za bima katika wilaya yetu bado kiko chini sana na hakuna mtu aliyewahi kufikiria kuwa wilaya yetu ingekumbwa na janga kama hilo,” Bi Mayanja alifafanua na kusema maafa hayo yamekuwa somo kubwa sana kwao.
“Kama tunataka kusonga mbele tukiwa na uhakika wa usalama wa maisha na mali zetu, wote sasa tunatakiwa kuanzisha utamaduni wa kuwa na kinga ya bima na kuzitumia bidhaa zake mbalimbali.”
Mmoja wa wanufaika wa fidia hiyo, Bi Hapiness Mlay, ambaye amelipwa TZS milioni 28.5, alisisitiza umuhimu wa hilo na kuwasihi wafanyabiashara wasiokuwa na bima kuhakikisha wanaipata ili kupunguza athari za kutokuwa na kinga hiyo.
Akibainisha kuwa ulipaji wa fidia kwa wakati ni takwa la kikanuni, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, amezichagiza kampuni za bima kulipa kipaumbele suala la unafuu wa gharama za huduma yanayozitoa.
“Hivi sasa, watoa huduma mbalimbali wa bima wamebuni bidhaa mbalimbali za bima ili kuwavutia watumiaji wengi. Natumia fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kuchangamkia fursa hii kikamilifu ili kupunguza athari za majanga,” alisema na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha utumiaji wa huduma hizo na kuzidi kupambania bima ya afya kwa wote.
No comments:
Post a Comment