HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 30, 2024

Amend, Uswiss wakabiliana na ajali kwa wanafunzi

Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga (DAS), Dalmia Mikaya (kushoto)wakifunua kitambaa baada ya kufanyika kwa uzinduzi wa mradi wa uwekezaji wa miundombinu ya usalama barabarani kwa shule za Msingi Azimio na Makorora Jijini Tanga ambao unaotekelezwa na Shirika la Amend Tanzania na kufadhiliwa na Ubalozi wa Uswis nchini.Kulia ni Mkurugenzi wa Amend Tanzania Simon Kalolo akiwa ameshika kitambaa wakati ukikatwa utepe.Wanaoshuhudia ni wadau wa masuala ya Barabarani kutoka Jiji la Tanga pamoja na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania

 

Na Mwandishi Wetu, Tanga

SHIRIKA la Amend kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uswiss wamejenga miundombinu salama ya barabara ili kuwawezesha wanafunzi wa Shule ya Msingi Makorora na Azimio jijini Tanga kuvuka kwa usalama barabarani wanapoenda shule.

Changamoto hiyo ya kuvuka barabara ilikuwa inawahusu wanafunzi zaidi ya asilimia 90 wa shule hizo ambao walikuwa katika hatari kubwa ya kugongwa na pikipiki, magari na vyombo vyengine vya moto.

Hayo yamebainishwa leo Mei 29,2024 jijini Tanga wakati wa uzinduzi wa mradi wa miundombinu salama ya barabara katika shule hizo ambapo viongozi wa ngazi mbalimbali wa Wilaya ya Tanga wamehudhuri huku wakionesha kufurahishwa na utekelezwaji wa mradi huo.

Mkurugenzi wa Shirika la Amend Tanzania Simon Kalolo amesema wamelazimika kujenga miundombinu hiyo ili kunusuru ajali kwa wanafunzi ambao wanatarajiwa kutimiza ndoto zao muhimu.

Kalolo amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wanafunzi wasiopungua 8 wa shule wamejeruhiwa kutokana na ajali za barabara zinazotokea kwa kukosekana alama za barabara na maeneo ya vivuko.

“Baada ya kushauriana na wadau wa shule hizo wakiwemo wanafunzi na walimu, jamii, viongozi wa dini, serikali za mitaa, Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) na Jeshi la Polisi, Amend kwa ufadhili Uswisi na tumeshirikiana kutekeleza mradi huu kwa kuweka vivuko pamoja na alama muhimu za barabarani,” amesema.

Amesisitiza kupitia mradi huo wameweka njia za waenda kwa miguu, matuta, vivuko vya pundamilia, alama za barabarani, na elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wote.“Tumezindua miundombinu mipya ya kuokoa maisha ya watembea kwa miguu hasa watoto wa shule hizi.”

Amesema katika Bara la Afrika watoto wako katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ajali za barabarani ikilinganishwa na eneo lingine lolote duniani na kufafanua bahati nzuri njia za kuzuia ajali hizo zinaeleweka.

Amesema mradi huo unaungwa mkono na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na una bajeti ya Sh.424,983,396 huku akifafanua mradi ulianza Septemba mwaka 2023 na shughuli zilizofanyika ni mafunzo kwa madereva bodaboda 300 katika Jiji la Tanga.

Pia madereva bodaboda 253 katika Jiji la Dodoma sambamba na kampeni ya uhamasishaji kuhusu masuala ya usalama wa pikipiki pamoja na kuanzishwa kwa 'Kanuni za Maadili' kwa waendesha pikipiki 200 ambao watapewa mafunzo jijini Tanga ifikapo Juni 2024.


No comments:

Post a Comment

Pages