HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 03, 2024

RC SINGIDA – TUTAKWAMUA UJENZI WA MAJENGO YA HOSPITALI YA RUFAA YA MANDEWA


Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego ameahidi kuwa atashughulikia haraka mkwamo wa ujenzi wa majengo Matatu katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Singida ya Mandewa likiwemo jengo la ghorofa Tatu linalotarajiwa kutoa huduma  za kibingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, wodi za watoto, huduma za wagonjwa mahutututi, maabara na huduma za ufamasia. 

Jengo hilo la ghorofa Tatu ujenzi wake alianza mwaka 2014 na kusimama kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mkandarasi aliyekuwa anajenga jengo hilo kusimamishwa kuendelea na ujenzi kutokana na uwezo mdogo katika utekelezaji wa mradi huo.

 

Mkuu wa mkoa Singida Halima Dendego ametoa kauli hiyo katika kikao chake na Watumishi wa Hospitali ya Rufaa na Mandewa ya mkoa wa Singida cha kusikiliza  kero na kukagua majengo ambayo ujenzi wake umesimama na kusisitiza kuwa  atalibeba jambo hilo na kulifanyia kazi ili ujenzi huo wa majengo hayo uweze kuendeleo haraka lengo likiwa ni kuongeza utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa mkoa wa Singida karibu na maeneo yao.

 

“Mimi ni Muumini ya Namba Moja kwa kila jambo hivyo nataka Hospitali hii ya Mandewa iweze kushika Namba nchini na Dunia kwa ujumla kwa utoaji huduma za kiwango cha juu za afya kwa wananchi kwani Hospitali nyingine wanaweza kwa nini sisi tushindwe na Serikali iwezesha vifaa na Watumishi wapo”Amesisitiza Halima Dendego.

 

Kuhusu watumishi wanaojitolewa kwa muda mrefu bila kupata ajira, Mkuu huyo wa mkoa wa Singida ameutaka Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa kumpatia orodha ya Watumishi wote wanajitolewa lakini hawajapata ajira ili aweze kuwasaidia katika ngazi husika.

 

Hata hivyo, Halima Dendego amewapongeza Watumishi hao kwa kufanya kazi kwa bidii bila kukata tamaa kutokana na kutopatiwa ajira na kusisitiza kuwa jambo atalishughulikia ili watumishi hao waweze kupata ajira za kudumu haraka.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Singida Martha Mlata amewasisitiza Watumishi wa hospitali ya Mandewa kuendelea kuchapa kazi bila kwa viwango vya juu kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inawajali na itaendeleo kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa muda muafaka.


Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa za mkoa wa Singida Dkt David Mwasota ameishukuru Serikali kwa kuwa bega kwa bega na Watumishi wa afya ikiwemo kuwapatia vitendea kazi vya kisasa na kuboresha maslahi yao hivyo jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi ili wasiende mikoa mingine kufuata huduma hizo za afya.

No comments:

Post a Comment

Pages