HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 08, 2024

SIMBA WANAJIKUNA UPELE KUMBE WANA KIDONDA

Na John Richard Marwa

Yawezekana muziki wa kileo hasa wa kizazi kipya haudumu sana kwenye Ngoma za masikio ya wasikilizaji ama wandewa wa muziki wenyewe.

Sio utunzi wala ala zinazopigwa kwenye huo muziki. Vipi Acha lizame ya Nandy akimshikirisha mtoto wa kimakonde Harmonize ndivyo unaweza kuelekea kinachoendelea mitaaa yenye pirikapirika nyingi ya Msimbazi kwenye Klabu ya Simba Mnyama wa mwituni inavyozama kila uchao.

Nasikia kelele zimekuwa nyingi sana mara oooh!  wajumbe  wa Bodi ya Wakurugenzi upande wa Mwekezaji kung'atuka ikiwa ni sehemu ya kuwajibika kwa matokeo mabaya na mwenendo wa misimu ya hivi karibuni.

Mara oooh Mwekezaji Mohamed Dewji amewataka wajiuzulu!! Kama Mwekezaji amewataka watu wake wajiuzulu kwa sababu ya matokeo na mwenendo mbaya wa timu kitendo ambacho wanachama na mashabiki wa Simba wameshangilia tukio hilo na kuona ni uwajibikaji huku wajumbe wa wanachama wao wakisalia na hakuna hatua yoyote inayonekana wao kuichukua.

Hapa ni sawa na kujikuna upele kumbe wana kidonda ambacho wanazidi kukichimba. Kwanini wanachama wafurahie wajumbe wa Mwekezaji kung'atuka na hawaoni haja ya kuwahoji wajumbe wao walio wachagua  kwanini timu yao inakwenda mrama.

Cha ajabu namsikiliza Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi upande wa wanachama Asha Baraka akisema haiwezekani kila timu itakapofungwa Viongozi wanapaswa kujiuzulu, mara hajui kamati ya usajili iko chini ya nani!!? Kichekesho hiki!

Utajiuliza kama Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi hajui kamati ya usajili, huwa wanaenda kufanya nini kwenye vikao? Mara anasema wajumbe wengine upande wa Mwekezaji wamekuwa hawahudhurii vikao maana yake mawazo yao na kumwakilisha Mwekezaji hakuko sawasawa.

Simba waache kujikuna kidonda, wakitibu ili wapone ugonjwa walionao kuliko kuendelea kukichimba kwa kucha na vidole vichafu.

Unaweza sema kinachoitafuna Simba hakijaanza leo bali tokea walipoanza mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo miaka kadhaa huko nyuma.

Niliwahi kuandika kwenye gazeti la Tanzania Daima enzi zake kuwa 'Mo Dewji ni Mwekezaji ama mpangaji Simba SC?'  ilikuwa kama siasa enzi za Mzee Kilomoni na kukatalia hati za umiliki wa klabu hiyo.

Ni wazi Simba walijipasua wenyewe wakiwa wamejichoma sindano ya ganzi.

Taarifa zinaendelea kuwa nyingi kila kukicha ndani ya viunga vya Msimbazi, hapa ndio unaikumbuka kauli ya Kocha Patrick Aussems kuwa Simba haitapiga hatua kwa sababu Ina baadhi ya viongozi ambayo hawana elimu ya mpira.

Hakuna kinachotokea kwa bahati mbaya kwa Wekundu wa Msimbazi kila mwanasimba anahusika kuifikisha hapa ilipofika aidha kwa kushiriki ama kwa kususia timu na kuwa watazamaji.

Nguvu ya Simba ni Nguvu Moja yaani kuanzia kwa mashabiki, wanachama, viongozi na wahafidhina wa Simba wakikaa pamoja na kuwa Nguvu Moja basi kidonda chao watapata dawa ya kukitibu na kutoka na kauli moja ya Nguvu Moja.



No comments:

Post a Comment

Pages