HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 01, 2024

WALIOTAFUNA FEDHA ZA MIKOPO YA HALMASHAURI SINGIDA KUSAKWA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego akizungumza kwenye kikao Maalum cha kujadili hoja za CAG katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Singida.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Serikali ya mkoa wa Singida imewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Polisi wa Wilaya mkoani humo kuwasaka na kuwakamata watu wote waliochukua mikopo ya asilimia 10 kwenye Halmashauri na kushindwa kuirejesha bila sababu za msingi.


Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego, ametoa kauli hiyo katika kikao cha Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Iramba cha kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Rc Dendego ametoa mfano kwa Halmashauri ya Iramba pekee zaidi ya Milioni 118 hazijarejeshwa mpaka sasa na kusisitiza kuwa tatizo lazima litafutia ufumbuzi kwa wahusika kukamatwa ili warejeshe mikopo hiyo.
“Nataka Dc na OCD muwasake popote walipo watu waliokopeshwa fedha hizo ili wazirejeshe ili wananchi wengine wakopeshwe,” Amesisitiza Dendego.
Ametaka wote wataokamatwa katika oparesheni hiyo wawekwe kizuizini na wasiachiwe mpaka hapo watakapolipa fedha hizo walizokopeshwa.
Mkuu huyo wa mkoa pia amewaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii mkoani humo washirikiane na Viongozi wengine katika kusaka Vikundi vilivyokopeshwa fedha hizo na kuzirejesha haraka vinginevyo tutazuia mishahara yao mpaka Vikundi hivyo vilipe fedha hizo kwa sababu wao wanavijua vikundi hivyo.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi, ameunga mkono hoja ya wanachama wa vikundi vilivyokopeshwa fedha za Halmashauri kusakwa ili warejeshe fedha hizo.
Msengi amesema fedha hizo zinazodaiwa ni nyingi hivyo lazima nguvu ya ziada itumike ili kuhakikisha waliokopeshwa wanazirejesha ili wananchi wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo.
Mwenyekiti huyo pia amemshukuru Rais Samia kwa kuipatia Halmashauri hiyo zaidi ya shilingi Bilioni Tatu kwa ajili ya kutelekeza miradi mbalimbali ya maendeleo hasa katika sekta za afya na elimu.

 

Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba  kikiendelea.

No comments:

Post a Comment

Pages