Na Miraji Msala, Dar es Salaam
Kampuni ya Skyruby, inayojihusisha na usambazaji wa vifaa vya uchimbaji madini, imeonesha ubora na weledi wake katika maonesho ya kimataifa ya MINEEXPO yaliyozinduliwa leo jijini Dar es Salaam, yakihusisha zaidi ya washiriki kutoka nchi 30 duniani.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Skyruby, Mayur Gavali, alisema kuwa ushiriki wa kampuni hiyo unalenga kujitangaza kibiashara, kuimarisha uhusiano wa kimkakati na kupata fursa ya kukutana na wawekezaji mbalimbali katika sekta ya madini.
“Kwa mwaka jana tulishiriki kwa mara ya kwanza na tuliona matokeo chanya. Mwaka huu ni mara ya pili kushiriki, na tumejipanga kufikia watu wengi zaidi kupitia maonesho haya yenye mvuto wa kimataifa,” alisema Gavali.
Aidha, Gavali alieleza kuwa MINEEXPO ni jukwaa muhimu linalowezesha kampuni za ndani na nje kubadilishana maarifa, kuonesha teknolojia mpya pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Biashara wa Skyruby, Mohit Adhe, alisema kuwa kampuni hiyo inaendelea kutekeleza mkakati wa kutoa huduma bora na za kisasa ili kuendana na mahitaji ya sekta ya madini ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Skyruby imekuwa ikijipatia heshima katika soko kutokana na huduma zake bora na vifaa vya kisasa vya uchimbaji, jambo linaloibua matumaini ya mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa sekta ya madini nchini.



No comments:
Post a Comment