MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC PL), wametanguliza mguu mmoja ndani kuelekea Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL), hii ni baada ya kuichapa Wiliete SC ya Angola kwa mabao 3-0 wakiwa ugenini.
Yanga wangeweza kuibuka na ushindi mkubwa zaidi kama wangekuwa makini katika kuzibadili nafasi walizotengeneza kuwa mabao, kwani walitawala mtifuano huo kwenye dimba la Novemba 11 (11 de Novembro), huku straika Prince Dube akikosa nafasi zaidi ya nne peke yake.
Mabao ya Yanga katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza yamewekwa kimiani na kiungo mkabaji Azizi Andabwile, winga mtokea benchi Edmund John na Dube, hivyo kuhitaji ushindi au sare ya aina yoyote wakati wataporudiana Septemba 27, ili kufuzu hatua inayofuata.
Iwapo watafanikiwa kuwatupa nje Wiliete SC katika marudiano ya mechi namba 22, Yanga SC watasubiri mshindi wa ujumla wa mechi namba 21 inayozikutanisha Association Sportive Elgeco Plus (ASSM Elgeco Plus) ya Madagascar dhidi ya Silver Strikers FC ya Malawi zinazoshuka dimbani Septemba 21 kucheza mechi yao ya kwanza.





No comments:
Post a Comment