NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibaha mjini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Silvestry Koka, amesema kuwa yupo tayari kuwatumikia wananchi kwa moyo wake wote endapo watamchagua tena, huku akiweka wazi mikakati yake ya kuleta maendeleo makubwa ndani ya siku 100 za kwanza.
Koka ameyasema hayo wakati wa mkutano wa kampeni kwa wananchi wa kata ya Tangini uliofanyika katika viwanja vya Loliondo,
Koka amesema lengo na dhamira yake kubwa ni kuhakikisha anawatumikia wananchi kwa vitendo ikiwa pamoja na kuwaletea chachu ya maendeleo.
“Ninakuja kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya. Najua changamoto zenu. Nipo tayari kuwatumikia kwa moyo mmoja na kuhakikisha tunasonga mbele pamoja,” alisema Koka huku akishangiliwa.
Katika kuboresha hali ya uchumi wa wananchi, Mhe. Koka alisema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 2 kimetengwa kwa ajili ya mikopo kwa wafanyabiashara wadogo ili kuwasaidia kukuza mitaji yao.
“Hii siyo ahadi ya kampeni tu, ni mkakati wa kweli. Tunataka mfanyabiashara mdogo awe mkubwa, bila kuandamwa na masharti magumu ya benki,” alisema koka.
Aidha, alisema serikali itahakikisha urasimishaji wa sekta zisizo rasmi unafanyika kwa kuwatengea maeneo rasmi ya biashara na kuanzisha mitaa ya viwanda.
Suala la Elimu Mhe. Koka alisema kuwa ndani ya siku 100, serikali itajenga madarasa saba na matundu ya vyoo 15 katika Shule ya Msingi Mamlaka ili kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora.
Kwa upande wa Shule ya Sekondari Tangini, aliahidi ujenzi wa matundu 12 ya vyoo pamoja na kupatikana kwa madawati 1,000 na viti ili watoto wasome kwa utulivu.
“Mtoto wa Kibaha Mjini ana haki ya kusoma katika mazingira mazuri kama wa Dar es Salaam au Dodoma. Elimu ni msingi wa maendeleo yetu,” alisema.
Pia, alibainisha kuwa ujenzi wa madarasa manne katika Shule ya Msingi Kilimahewa umeanza kwa kutumia shilingi milioni 300 zilizotolewa tayari, huku lengo likiwa ni kupunguza msongamano na kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Sekta ya Afya,Koka alisema zahanati ya Tangini ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, huku zahanati ya Kilimahewa ikiwekewa mkakati wa kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya, ambapo shilingi milioni 90 zimetengwa kwa ajili ya vifaa tiba.
“Afya ya mwananchi ni kipaumbele. Hatuwezi kuwa na taifa imara bila watu wenye afya bora,” alisema koka.
Aliahidi pia kuboresha Hospitali ya Manispaa ya Lulanzi kwa kujenga uzio na njia za kupitisha wagonjwa, pamoja na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa bei nafuu kupitia maduka ya serikali.
Maji Safi na Barabara Zaidi Za Lami Katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji, Koka alieleza kuwa mradi wa ujenzi wa tanki kubwa la maji utaanza katika maeneo ya Kilimahewa na Tangini, huku mabomba ya maji ya urefu wa kilomita 4 yakisambazwa kutoka Kata ya Benki hadi Bandari.
Aidha, alibainisha kuwa kiasi cha shilingi milioni 420 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara zilizoharibiwa na mvua za hivi karibuni.
“Barabara si anasa, ni msingi wa uchumi. Tutahakikisha kila mtaa unapitika, hata kwa wakati wa mvua,” alisema.
Alisema mkataba wa shilingi bilioni 17.11 umesainiwa tayari kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami katika maeneo ya Pangani, Mitamba, Mnarani, Msufini, Tangini na maeneo ya KCCC.
Soko Kuu la Kisasa na Fursa za Mikopo kwa Vijana Mhe. Koka aliahidi kujenga soko kuu la kisasa katika Manispaa ya Kibaha litakalogharimu shilingi milioni 800, ambalo litakuwa kitovu cha biashara kama ilivyo Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Sambamba na hilo, alisema asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zitaelekezwa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia mikopo isiyo na riba.
Kwa upande wake, mgombea udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM)wa Kata ya Tangini, Anthony Milao, aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuahidi kushirikiana na wananchi katika kutatua kero zote.
“Tutahakikisha elimu, miundombinu na uchumi vinapewa kipaumbele. Hakutakuwa na mtu wa pembeni. Kila mmoja ataonja matunda ya maendeleo,” alisema Milao.
Pia, Mhe. Koka alisisitiza kuwa hana sababu ya kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa sababu anawajua wananchi wake na mahitaji yao.
“Nipo tayari kutembea nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa, kuhakikisha tunajenga Kibaha Mpya. Nitakuwa mtumishi wenu, si bosi wenu. Nia yangu ni moja maendeleo kwa wote,” alisema koka.
October 04, 2025
Home
Unlabelled
KOKA AAHIDI KUTATUA KERO NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WANANCHI KATA YA TANGINI
KOKA AAHIDI KUTATUA KERO NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WANANCHI KATA YA TANGINI
Share This
About HABARI MSETO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Author Details
Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.



No comments:
Post a Comment