HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 04, 2025

Serikali: Hatujaufunga Benjamin Mkapa, acheni upotoshaji

SERIKALI ya Tanzania imevunja ukimya kwa kutoa ufafanuzi wa madai iliyoyaita ya upotoshaji kuwa imeufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kipindi cha miezi sita, kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.

‎Ufafanuzi huo umetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ambaye ameenda mbali kwa kuwajibu wanaohoji kuhusu ukarabati wenye thamani ya Sh. Bil. 31 uliofanyika uwanjani hapo.

‎Katika taarifa yake ya ufafanuzi kwa umma wa Watanzania hususani wapenda kabumbu, Msigwa amesema: "ACHENI KUPOTOSHA. Hatujatangaza kuufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa miezi 6 kama baadhi ya watu wanavyopotosha.

‎"Tumekaa na TFF na pia timu za Yanga na Simba zilioomba kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mechi za ligi na kufanya tathmini ya uharibifu wa sehemu ya kuchezea (pitch) ya uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya mechi mfululizo zilizopita za Kimataifa na za ligi.

‎Ukarabati huo unakuja baada ya dimba hilo kutumika kwa michezo ya Simba Day, Yanga Day, Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Wiliete Benguela ya Angola na Ile ya Simba dhidi ya Gaborone United ya Botswana. 

‎Lakini pia dimba hilo limetumika kwa mechi mbili za Ligi Kuu za Simba na moja ya Yanga, mechi zote hizo nane zikipigwa katika kipindi cha wiki sita hadi saba kuanzia Agosti 10 hadi Septemba 28.

‎"Tumekubaliana kuwa Yanga na Simba watafute viwanja vingine kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu na Uwanja wa Benjamin Mkapa ubaki kwa ajili ya mechi za Kimataifa, Timu ya Taifa na Dabi, mpaka hapo tutakapofanya ukarabati mkubwa wa 'pitch," amesema Msigwa.

‎Kuhusu Ukarabati wa Sh. Bil. 31, Msigwa amesema: "Wale wanaohoji Bilioni 31 zilizotumika kukarabati uwanja, ni hivi ukarabati huo haukuhusisha ukarabati wa pitch. 

‎"Ulihusisha kuboresha jengo, kuweka mifumo mipya ya umeme na taa, maji, vyoo, njia ya kukimbilia, kuweka viti vyote 62,000, kuweka viyoyozi, mfumo wa sauti, ubao wa matangazo, mabenchi ya ufundi, magoli, kupaka rangi na mfumo wa sauti.

‎"Walioingia Uwanja wa Benjamin Mkapa nambieni kipi hakijafanyika kati ya hivyo?," amehoji Msigwa.

‎Akaongeza kwamba, ni vizuri pia kujua kuwa uwanja mkubwa kama Benjamin Mkapa kila unapotumika ni lazima ufuatiwe na marekebisho, kwa sababu hakuna tukio linaloweza kufanyika bila kusababisha uharibifu. 

‎"Na hii sio kwa uwanja huu tu ni viwanja vyote Dunia, na ukarabati wake unahitaji utaalamu na sio kubondabonda.

‎"Kumbukeni kulingana na maelekezo ya kitaalamu ya matumizi sahihi ya uwanja wa nyasi halisi (natural grass) uwanja unapaswa kutumika mara mbili au tatu tu kwa wiki. Hope tumeelewana. #KaziIendelee," amemaliza Msigwa. 



 

No comments:

Post a Comment

Pages