HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 13, 2025

Dkt. Mwinyi azindua Bodi ya Wakandarasi Z'bar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameizindua Jumuiya ya Wakandarasi wa Sekta ya Ujenzi Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote wa sekta hiyo kutokana na umuhimu wake katika utekelezaji wa mipango ya Serikali.


Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 11 Septemba 2025, wakati akiizindua jumuiya hiyo katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Aiport, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amefahamisha kuwa katika miaka ya karibuni Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya ujenzi kwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, skuli na hospitali, hivyo kuanzishwa kwa jumuiya hiyo kutatoa fursa ya ushirikiano, mijadala na taaluma baina ya Serikali na wadau katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi.


Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza hatua ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo, akieleza kuwa ni chombo muhimu cha kuwasilisha changamoto, ushauri na mapendekezo kwa Serikali yatakayosaidia kuimarisha sekta ya ujenzi nchini.


Ameeleza kuwa sekta ya ujenzi Zanzibar imefungua historia mpya kwa kuleta ushirikiano kati ya wadau wa ujenzi na Serikali kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.


Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia wadau kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na jumuiya hiyo ili iendelee kutoa mchango wake katika kuimarisha sekta hiyo na kukuza sekta nyengine za kiuchumi nchini.


Kuhusiana na changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wadau, ameiagiza Wizara ya Ujenzi pamoja na Bodi ya Wakandarasi kuwaunganisha wadau na taasisi za kifedha ili kupata mikopo, sambamba na kuangalia uwezekano wa kuandaa mifuko maalum ya kuwasaidia wadau wa sekta hiyo.


Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza wadau hao kuwa na umoja, mshikamano na kuepuka migogoro isiyo na tija, kwa kuwa wana wajibu wa kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya ujenzi.

 

No comments:

Post a Comment

Pages