HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 01, 2025

MKOA WA PWANI BALAA WAENDELEA KUNG’ARA KATIKA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASIKINI (TASAF)

NA VICTOR MASANGU, PWANI 

Katibu Tawala Msaidizi wa uchumi na uzalishaji kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala amewahimiza  waratibu wa Mpango wa Kunusuru kaya masikini (TASAF) kuhakikisha vikundi vilivyoundwa na kunufaika na mpango wa TASAF awamu ya pili vinasimamiwa vizuri, na kupatiwa  elimu na  mitaji kupitia mikopo  ya asilimia 10  ili kuweza kupambana na wimbi la umasikini na kujikwamua kiuchumi.


Twamala ametoa kauli hiyo  wakati akifungua kikao kazi cha mwaka cha utekelezaji  wa Mpango huo wa  (TASAF)  awamu ya pili kwa kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ambacho kimefanyika  katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Aidha ameishukuru serikali kwa kuweza  kwa kutoa  zaidi ya Bilioni 44 kwa ajili ya uwendeshaji na kuwezesha miradi mbalimbali kutokana na  mapango huo kuweza kuzinufaisha familiiza mbali mbali za ya hali chini kwa kiasi kikubwa.

Pia amesisitiza kwamba  miradi ambayo  haijakamilika ikamilike kwa wakati ili kuweza  kutendea haki serikali pamoja na kuwanufaisha wananchi.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Mkurungezi  Kutoka Makao Makuu ya TASAF Eng. Abel Bimbiga ambaye pia  ni afisa miradi ameupongeza kwa dhati Mkoa wa Pwani kwa kuweza  kutekeleza miradi kwa ufanisi na kuweza  kubadilisha maisha ya kaya ambazo ni masikini.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji Mratibu wa TASAF Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, amesema kwamba  Mkoa wa Pwani ulikuwa miongoni mwa maeneo ya mwanzo yaliyochaguliwa kwa ajili ya majaribio ya awali ya mpango huo, ambapo Wilaya za Bagamoyo na Kibaha ziliteuliwa kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza.


Amesema kuwa Mkoa wa Pwani   umenufaika na utekelezaji wa  miradi ya afya na elimu  16 na kubainisha baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na  Jengo  la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya Msoga, wodi ya mama na mtoto Miono Chalinze, Zahanati ya mwanalugali , nyumba za watumishi Zahanati ya Vikawe Manispaa ya kibaha , Majengo 5 kituo cha afya Nyamatanga Kibiti, Bweni la wasichana na nyumba za walimu Shule ya Sekondari Samia  Rufiji.

Kimaro amesema kuwa kufuatia mafanikio yaliyoonekana katika hatua ya majaribio, Serikali ilipanua mpango huo hadi kufikia wilaya zote na mikoa 26 nchini kote, ili kuhakikisha kuwa wananchi wengi zaidi wananufaika na juhudi za kupunguza umaskini ambapo miradi mbalimbali ilitekelezwa.


Kwa mujibu wa Kimaro, hadi kufikia Juni 2025, Mkoa wa Pwani ulikuwa umefanikiwa kuunda jumla ya vikundi 1,601 vya wanufaika wa TASAF, vyenye wanachama 16,495. Kati ya hao, wanawake ni 14,568 na wanaume 1,927. Kupitia vikundi hivyo, wanufaika wamewezeshwa kuanzisha miradi ya kiuchumi, kuweka akiba, na kujitegemea kiuchumi.

Aidha, wanufaika wamepata mafanikio makubwa katika huduma za msingi kama elimu, afya, lishe na makazi bora ikiwa na wamenufaika kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji, usindikaji wa bidhaa, biashara ndogondogo, pamoja na ujasiriamali wa ushonaji na ufumaji.

 Jumla ya mtaji wa vikundi hivyo umefikia shilingi milioni 330 hadi sasa.

Mratibu huyo amebainisha kuwa lengo la Serikali kupitia TASAF si kutoa misaada ya muda mfupi pekee, bali kuwawezesha walengwa kuwa na msingi madhubuti wa kiuchumi, utakaowasaidia kujitegemea hata baada ya mpango kumalizika.

 Ameongeza kuwa vikundi hivyo pia vinatarajiwa kukidhi vigezo vya kupata mikopo ya asilimia 10 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri zao.
Kimaro alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, viongozi wa jamii na wanufaika wenyewe. 

Katika hatua nyingine ameweka bayana kuwa mpango huu utaendelea kubadilisha maisha ya wananchi wengi na kuchochea maendeleo endelevu ya Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.

Mkoa wa Pwani umeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ambao ulianza kutekelezwa nchini tangu mwaka 2014 kwa lengo la kupunguza umaskini uliokithiri na kuinua hali ya maisha ya wananchi wa kipato cha chini.






No comments:

Post a Comment

Pages