Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Wakati Watanzania wakielekea katika tukio la Kikatiba la kupiga kura mnamo Oktoba 29 mwaka huu, Muunganiko wa Asasi za Kiraia zinazotetea makundi maalum ikiwamo wanawake, watoto na wenye ulemavu umeungana kuhimiza umma kuhusu ajenda muhimu ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, sambamba na kuhimiza wanawake kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo.
Wakizungumza na wanahabari Jijini humo leo wanawake viongozi kutoka asasi hizo wamewaambia wanahabari kuwa ushiriki wa wanawake katika siasa unachochea uwepo wa viongozi wanawake.
Rose Haji Mwalimu ambaye ni Mwanzilishi na Mwakilishi wa Tamwa akilisoma tamko hilo kwa niaba ya muunganiko huo,amesema kuwa Kwa mujibu wa asasi hizo, ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ni miongoni mwa vipaumbele vya mashirika yenye mrengo wa kijinsia, kwani uwepo wa viongozi wanawake huchochea utekelezaji wa hatua mahsusi za kuongeza kipato na maendeleo ya wanawake nchini.
“Asasi zetu zinahimiza wanawake kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi ili tuweze kuwachagua viongozi watakaosimamia ajenda za msingi zinazowagusa wanawake, watoto, vijana wanawake na watu wenye ulemavu,” amesema.
Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika kukuza ushiriki wa wanawake katika uongozi, ikioneshwa na historia ya kuwa na Rais wa kwanza mwanamke, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, anayewania tena urais kwa tiketi ya CCM mwaka huu. Aidha, uchaguzi wa mwaka 2025 umeonesha ongezeko la wagombea wanawake wa urais akiwemo Saumu Rashid (UDP) na Mwajuma Mirambo (UMD).
Vilevile, wagombea wenza wa urais wanawake wametajwa kuwa ni pamoja na Eveline Wilbard Munis (NCCR), Husna Mohamed Abdallah (CUF), Aziza Haji Selemani (Demokrasia Makini), Amani Selemani Mzee (TLP), Chausiku Khatibu Mohamed (NLD), Sakia Mussa Debwa (SAU), Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja (CHAUMA)
Asasi hizo zimeeleza kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa ya kidemokrasia na ushahidi wa kuimarika kwa ajenda ya usawa wa kijinsia nchini. Zimewataka Watanzania kutambua kuwa mwanamke kiongozi asihukumiwe kwa jinsia yake bali kwa uwezo, dira, na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
“Uongozi wa mwanamke si tishio bali ni nyenzo ya kuimarisha demokrasia jumuishi,” wamesema.
Tamko hilo limekemea vikali lugha za kejeli, udhalilishaji na mashambulizi ya kibinafsi dhidi ya wagombea wanawake katika kipindi cha kampeni, likitaka mjadala wa kisiasa ujikite katika sera, hoja na ilani za maendeleo badala ya misingi ya kijinsia.
Aidha, asasi hizo zimepongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia katika kuimarisha usawa wa kijinsia, hususan kupitia mageuzi ya kisheria na miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo sekta ya afya. Zimeeleza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kuendelezwa kwa vitendo kupitia ushiriki endelevu wa wanawake katika maamuzi ya kitaifa.Zimeikumbusha pia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa na wadau wengine kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki salama, huru na jumuishi dhidi ya vitisho, ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Hata hivyo kupitia asasi hizo,Vyombo vya habari vimehimizwa kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake kushiriki midahalo na mijadala ya kisiasa ili kujenga uelewa wa umma kuhusu uwezo na mchango wa wanawake katika maendeleo.
Kwa kumalizia, muunganiko huo wa asasi za wanawake na watetezi wa usawa wa kijinsia umesisitiza:
“Uongozi bora hauna jinsia — ni dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi. Taifa lenye usawa wa kijinsia ni taifa lenye amani, ustawi na maendeleo endelevu.”amesema
Miongoni mwa asasi zilizoungana kutoa tamko hilo ni pamoja na Ulingo wa wanawake,Women welfare Tanzania,Wajiki,Wildaf, WFT,Young and alive,Generation act,TAWIA,Binti Makini na TAMWA.
Hata hivyo wananchi wa Tanzania bara na upande wa Visiwani Zanzibar wanatarajia kuchagua viongozi kwa ngazi za Udiwani,Ubunge na Rais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu.




No comments:
Post a Comment