HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 17, 2025

Tunguu-Makunduchi kuwa njia nne

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar


MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi  amesema  serikali inakusudia kukamilisha ujenzi wa barabara ya njia nne ya Tunguu hadi Makunduchi  pamoja na barabara  za  ndani Katika Mkoa wa Kusini  Unguja.




Rais Dkt Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza katika mkutano wa kampeni  uliofanyika uwanja wa michezo wa Paje,  Mkoa wa Kusini Unguja.


Mradi mwingine ameutaja kuwa ni ujenzi wa madaraja kwa ajili ya kuiunganisha mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja  kwa ujenzi wa daraja la Unguja Ukuu- Uzi Ng'ambwa unaoendelea pamoja na wa daraja la Chwaka hadi Charawe.


Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi  ujenzi wa  bandari ya Kizimkazi pamoja na kuziimarisha bandari ndogo za Mtene, Chwaka na Unguja Ukuu na wa  kiwanja cha ndege cha Nungwi na kiwanja cha Paje na kuelezea kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaufungua mkoa wa Kusini kiuchumi na ustawi wa jamii.

Rais  Dkt. Mwinyi alisema serikali itajenga madarasa mapya katika mkoa wa kusini  ikiwemo madarasa 1000 kwa shule za msingi na mengine 1000 kwa za Sekondari  utakaombatana na shule za msingi nne  na kumi za sekondari zote zikiwa za ghorofa.


Kuhusu sekta ya afya alisema serikali inajipanga  kujenga hospitali  ya  mkoa wa Kusini Unguja  wakati tayari ikiendelea na ujenzi wa Hosptali ya  Rufaa ya kufundishia ya  Binguni na Hospitali Kutibu Saratani ya Binguni na kuhusiana na suala la maji ameeleza kuwa serikali  inajipanga kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika mkoa huo utakaogharimu  Dola za Marekani Milioni 55, Mradi utakaomaliza tatizo la Maji Mkoani humo.


Ameyataja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni  Uroa, Marumbi, Pongwe, Jambiani na Makunduchi.


Eneo jingine ni kuwawezesha wanachi kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kutendea kazi, mikopo isio na riba na kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi zao kwa wajasiriamali.  


Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza kuwahimiza wananchi umuhimu wa kudumisha amani wakati huu kuelekea  Uchaguzi na baada ya uchaguzi  kwani ndio nyenzo muhimu ilioiwezesha  serikali kutekeleza miradi mingi ya maendeleo  katika miaka minne iliopita.


Mgombea huyo wa CCM kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar amewaomba wananchi kumchagua tena kuiongoza Zanzibar ili aendelee kuleta maendeleo makubwa zaidi chini ya Kaulimbiu yake ya "Yajayo ni neema zaidi'.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar  Dkt, Muhammed Said Dimwa amemuelezea Dkt. Mwinyi kuwa kiongozi muadilifu, mkweli na mwenye hekima katika utendaji wake na kuwaomba wananchi  kumchagua tena kuiongoza Zanzibar  kwa mafanikio zaidi.

No comments:

Post a Comment

Pages