Serikali
kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kuboresha usimamizi wa
hifadhi ya mazingira ili kuwaondolea wakazi wa Kilosa na maeneo mengine adha ya
mafuriko ya mara kwa mara.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu
wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange wakati alipopewa nafasi
na Waziri Mkuu Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba awasalimie wakazi wa Tindiga wilayani
Kilosa mkoani Morogoro leo Januari 02, 2026 baada ya kukagua athari za mafuriko
kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Dkt. Dugange amesema tayari Serikali ngazi ya
Taifa, Mkoa na Wilaya imeshaanza utekelezaji wa mpango wa utunzaji wa mazingira
kwa kusimamia zoezi la upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuongeza kasi ya
upandaji wa miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha
kutokea kwa mafuriko.
Alisema kuwa ni wakati sasa kila mwananchi awe
anachukua jukumu la kupanda miti angalau mitano kwa mwaka na kuitunza, hatua
itakayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
.jpg)
Naibu Waziri Dkt. Dugange alielezea umuhimu wa
upandaji miti na kubainisha kuwa maeneo yanapokosa miti ya kutosha, mvua
inaponyesha husababisha mafuriko.
"Ukweli ni kwamba bado kasi ya upandaji wa
miti inahitajika, mafuriko haya ndugu zangu Wana-Tindiga yanatokana na mito
yetu kuwa na kina kifupi, mvua zikinyesha maji yanatapika yanakuja kwenye
makazi ya wananchi na kuleta madhara makubwa, madhara ya kupoteza maisha,
kuharibu miundombinu kwenye kilimo, kuharibu vituo vya huduma na makazi ya
watu," alisema.
Pia, Dkt. Dugange alisema kuwa miongoni mwa
nguzo zilizomo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025-2050) ni Uhifadhi wa
Mazingira na Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ambayo inahitaji nguvu za
pamoja ili kufikia shabaha ya uboreshaji wa mazingira hasa kwa kupanda miti kwa
wingi.
Katika salamu hizo, Mhe. Dkt. Dugange aliungana
na Mhe. Waziri Mkuu kutoa pole kwa wananchi wa Tindiga na Wilaya ya Kilosa kwa
ujumla kutokana na madhara ya mafuriko yaliyotokea.


No comments:
Post a Comment