HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

March 28, 2026

RAIS SAMIA AONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MWILI WA LUKUVI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza viongozi wa kitaifa, familia, na wananchi kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.



Rais Dkt. Samia amesema Taifa limepoteza kiongozi mwenye uzoefu mkubwa na aliyetoa mchango wa muda mrefu katika utumishi wa umma, akimtaja Marehemu Lukuvi kuwa miongoni mwa viongozi waliolitumikia Taifa kwa uzalendo, bidii na uadilifu. 


“Tumeondokewa na kiongozi wetu, ndugu yetu na mtumishi mwenzetu aliyejitolea maisha yake kwa Taifa. Msiba huu si wa familia pekee bali ni wetu sote Watanzania, kwa sababu wengi waliguswa na mchango wake katika utumishi wa umma,” amesema Rais Dkt. Samia.



Aidha, Rais Dkt. Samia amesema Marehemu Lukuvi atakumbukwa kwa busara zake, uzoefu mkubwa wa uongozi na mchango wake katika kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali, ikiwemo kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kushughulikia changamoto za wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.


Ameongeza kuwa Taifa limempoteza Marehemu Lukuvi katika kipindi kilichohitaji uzoefu, hekima na ushauri wake, hususan katika wakati uliopo wa changamoto za kiuchumi na kisiasa duniani. 



“Katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, tulimhitaji ndugu Lukuvi zaidi kuliko wakati wowote kutokana na uzoefu wake mkubwa katika uongozi wa Taifa,” amesema Rais Dkt. Samia na kuongeza kuwa utumishi wake unabaki

kuwa mfano wa uongozi wa kujitolea, na kuwaasa viongozi na watumishi wa umma kuendeleza misingi ya uwajibikaji, uzalendo na kujitoa kwa manufaa ya Taifa.



Rais Dkt. Samia pia amesema Marehemu Lukuvi alikuwa kiongozi aliyegusa maisha ya wananchi wengi kupitia mtindo wake wa uongozi wa kusikiliza, kushauri na kuchukua maamuzi kwa maslahi ya Taifa. Ameeleza kuwa uzoefu wake wa muda mrefu katika nyadhifa mbalimbali za Serikali, Bunge na Chama cha Mapinduzi ulimfanya kuwa miongoni mwa viongozi waliokuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha utendaji wa Serikali.


Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa utumishi wa Marehemu Lukuvi ni kielelezo cha uongozi wa kujitolea, akibainisha kuwa viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kuendeleza misingi ya uwajibikaji, uzalendo na kujitoa kwa manufaa ya Taifa kama alivyofanya Marehemu katika kipindi chote cha utumishi wake.



Awali, akisoma wasifu wa Marehemu, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi, amesema Marehemu Lukuvi, aliyeshika nyadhifa mbalimbali za uongozi enzi za uhai wake, alitambulika kwa uchapakazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan katika kuratibu shughuli za Serikali, na kuongeza kuwa atakumbukwa kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na Bunge.


Ibada ya kuaga pia imehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na viongozi wengine wakuu na wastaafu wa Serikali, sekta binafsi, vyama vya siasa, viongozi wa dini, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Pages