Hali ya Usalama nchini inaendelea vizuri kutokana na jitihada za Jeshi la Polisi zinazo saidiwa na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi katika kubaini na kuzuia uhalifu.
Pamoja
na ushwari huo, yapo matukio mengine yanatendeka kutokana na matumizi mabaya ya
mitandao ya kijamii yakiwepo ya utapeli ambayo yameendelea kudhibitiwa.
Matukio
hayo ya kitapeli ni yale ambayo taarifa zake zimetolewa na baadhi ya wananchi katika Vituo vya Polisi
wakilalamika kutapeliwa kupitia mitandao ya kijamii. Taarifa hizo zimeonyesha
matapeli wanaofanya uhalifu huo kupitia mitandao ya kijamii wamekuwa wakitumia
njia mbalimbali kulaghai watu.
Miongoni
mwa njia za kilaghai au za kitapeli wanazotumia ni kama vile kutuma jumbe
zinazosema "ile fedha tuma kwenye namba hii" ingawaje njia hii na
ulaghai huu umeendelea kupungua kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada
zinazofanikisha kukamatwa kwa wahalifu waonatumia ulaghai wa aina hiyo na
kufutwa au kuondolewa kwa namba za simu walizokuwa wanatumia kwenye mfumo wa
mawasiliano.
Njia
zingine wanazotumia matapeli ni pamoja na kutuma ujumbe wakilaghai ukionyesha
umetumwa na kampuni fulani ya simu ukisema; "Huduma zako zote
za....zinafungwa leo tarehe....kwa kukosa kurasimisha na kuhakiki namba yako.
Kwa msaada piga ofisi zetu za....kwa namba hii "
Anayetumiwa ujumbe kama huo akipiga namba aliyotumiwa ndipo
maneno ya kitapeli yakiwemo ya vitisho kuwa simu yako itafungiwa huanza ikiwepo
kuambiwa
afungue viunganishi anavyotumiwa (links) na baadaye huambiwa kuingiza namba
yake ya siri/neno siri na akihadaika na kufuata maelekezo anayopewa na kuiingiza neno siri
ndipo hujikuta ameibiwa fedha zake. Lakini pia matapeli hutumia njia nyingine
ya kumwambia anayetapeliwa atume kiasi cha fedha ili namba yake isifungiwe.
Pia,
matapeli wengine wamekuwa wakitengeneza akaunti bandia na matangazo kisha
kuyasambaza kwenye mitandao wakitumia majina ya Viongozi wa Serikali na Majina
ya Wafanyabiashara wakubwa na makampuni yao wakijifanya kuwa, viongozi na wafanyabiashara hao wameanzisha utaratibu wa
kukopesha mikopo yenye riba nafuu.
Haya
yote yanakuwa na malengo
ya kutapeli na kuwaibia watakao
jiingiza katika mtego huo.
Wanaovutiwa na mtego huo huambiwa watume kiasi fulani cha kulipia gharama za
kuandaa mkopo huo. Anaye laghaiwa akituma kiasi hicho cha fedha alicho ambiwa,
anakijikuta mkopo hapati na anapo jaribu kuwasiliana na aliyekuwa anawasilia
naye anakuwa hapatikani tena na simu aliyokuwa anatumia haipo hewani imefungwa.
Tahadhari
inatolewa kwenu kujihadhari na utapeli wa aina hii na tuendelee kuelimishana
kuwa, viongozi wa serikali au wafanyabiashara wakubwa hawawezi kuanzisha
makampuni ya kukopesha yasiyokuwa na ofisi maalum zinazojulikana na wala zinazo
mtaka mkopaji alipie kiasi fulani cha fedha kwanza
ndipo apewe mkopo.
Aidha,
upo utapeli mwingine unao endelea kupitia mitandao ya kijamii ya matapeli
kujifanya kuwa, wanauza bidhaa fulani na hutuma picha kwenye mitandao za bidhaa
wanazouza tena kwa bei ambayo ni rahisi kuliko bei za makampuni au
wafanyabiashara wanaouza bidhaa kama hizo.
Ulaghai
wanaotumia ni kumtaka mhitaji wa bidhaa walizo tuma picha kwenye mitandao
awatumie kiasi fulani cha fedha ndipo wawatumie bidhaa husika na akishapokea
bidhaa ndipo amalizie kulipa kiasi kilichobakia. Waliofika katika Vituo vya
Polisi wameeleza walipotuma kiasi hicho cha fedha walicho ambiwa ndipo
walibaini walikuwa wametapeliwa kwani namba aliyokuwa anawasiliana nayo
hutoweka na haipatikani tena. Tuchukue tahadhari kubwa sana pale tunapotaka
kufanya biashara kupitia mitandao kwa kuhakikisha ni mtu au kampuni halali na
sahihi unafanya nayo biashara.
Hivyo,
Jeshi la Polisi lingependa kuendelea kutoa tahadhari kwa wananchi kujihadhari
na utapeli unaofanywa na matapeli wa mtandaoni na kikubwa kuendelea kupeana
elimu kuanzia wanaoishi mijini hadi vijijini juu ya utapeli wa aina hizo kwani
ndiyo njia pekee na nzuri ya kujikinga na uhalifu na wahalifu wa aina hii.
Jeshi
la Polisi litaendelea kutimiza wajibu wake wa kuwasaka na kuwakamata wahalifu
wanaojihusisha na uhalifu wa aina yeyote ile na kuwachukulia hatua za kisheria
na kwa upande wa wananchi tunatoa wito waendelee kupeana elimu na kuchukuwa
tahadhari kabla ya kufanya maamuzi na kamwe tusiongozwe au kusukumwa na tamaa
au uharaka wowote ili kujiepusha na mitego ya matapeli mitandaoni.




No comments:
Post a Comment