Na Antonia Mbwambo, Arusha
Watumishi
wa Umma nchini wamehakikishiwa kuboreshewa mazingira ya kazi kadri uchumi
utakavyoruhusu ili kuleta tija katika utendaji kazi kwa maslahi ya umma.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika leo
tarehe 12 Mei, 2026 katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Mhe. Qwaray amesema, Serikali
inatambua na kuthamini mchango wa Watumishi wa Umma wote nchini wakiwemo
Wauguzi, hivyo itazingatia changamoto wanazokutana nazo watumishi hao, pamoja
na kushughulikia
kwa uzito unaostahili ili kutengeneza mazingira mazuri ya
utendaji kazi.
"Niwahakikishie Serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya Watumishi wa Umma kadri
uchumi utakavyoruhusu kwani tunatambua mchango wenu mkubwa katika kuwahudumia Watanzania,
fanyeni kazi, Serikali ipo nanyi." Mhe. Qwaray alisema.
Aidha
Mhe. Qwaray ameongeza kuwa, ili kuwa na
ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi Serikali itaendelea
kuisimamia sekta ya afya pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma bila
kuathiri misingi ya Utumishi wa Umma, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa
ikiwemo uzingatiaji wa maadili.
Aidha amewataka kuwa na kauli
nzuri, huruma na upendo utakaoongeza tija
katika utendaji kazi ili kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya afya.
Ninyi ndiyo watu wa kwanza kukutana
na mgonjwa pindi anapofika hospitali na ni watu wa mwisho mgonjwa anapotoka
hospitali baada ya matibabu, ikiwa mtakuwa na nyuso za
ukatili na ulimi mkali au wa kebehi, mtawakwaza wagonjwa na hata kuwakatisha
tamaa jambo ambalo litaonyesha mapungufu katika sekta ya afya.”Mhe. Qwaray
alisema.
Vilevile, Mhe. Qwaray
amewaahidi Wauguzi hao kuwa Ofisi imepokea masuala yote waliyoyaeleza katika
risala yao na kuwaahidi kuyawasilisha kwa ajili ya kufanyiwa kazi ikiwemo masuala ya Muundo Mpya wa Utumishi wa Kada ya Uuguzi na Ukunga na Muundo
wa Utawala katika Sekta ya Afya ili kuboresha huduma ya afya na maslahi ya watumishi wa afya nchini.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Qwaray, ametoa wito kwa wauguzi kuhahakisha wanabadili mienendo na tabia
zisizopendeza wala kuendana na maadili ya kazi yao, lakini pia amewapongeza kwa
jitihada kubwa wanazozifanya katika kuwahudumia wananchi na kuboresha afya zao.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wauguzi
(TANNA), Dkt. Ezekiel
Mbao amemshukuru Naibu Waziri, Mhe.
Regina Qwaray kwa kujumuika nao kwenye maadhimisho ya siku hiyo adhimu.
Maadhimisho
hayo ya Siku ya Wauguzi Duniani yamebeba kauli mbiu isemayo “Wauguzi Wetu, Mustakabali
Wetu, Wauguzi Waliowezeshwa Huokoa Maisha.”




No comments:
Post a Comment