NA DENIS MLOWE, IRINGA
MGOGORO wa umiliki wa shamba namba 1135 lililopo kijiji cha Magunga, Wilaya ya Iringa ulioingiliwa na baadhi ya wananchi licha ya kumilikiwa kihalali na kampuni ya Iringa Food and Beverages Ltd umeamua kutoa ufafanuzi wa chanzo cha mvutano unaoendelea baina ya mmiliki na wanakijiji.
IFB imetoa ufafanuzi kupitia kwa wakili wao, Innocent Boniface ambaye ameeleza historia kamili ya umiliki wa ardhi hiyo pamoja na chanzo cha mvutano unaoendelea unaosababishwa na baadhi ya viongozi wa kijiji.
Kwa mujibu wa maelezo ya wakili Boniface, shamba hilo lilinunuliwa na wateja wake kutoka kwa wamiliki wawili wa awali. Mmiliki wa kwanza Joshua Nyangoya, aliyemiliki Shamba Na. 102 lenye jumla ya ekari 200. Mmiliki wa pili alikuwa Godliven Joshua Mandari, aliyemiliki Shamba Na. 83 lenye takribani ekari/hekta 200.
Mashamba yote mawili yalikuwa yamemilikishwa kihalali na mamlaka husika shamba la Joshua Nyangoya lilitolewa hati tarehe 10 Machi 1989, na lile la Godliven Mandari likitolewa hati tarehe 36 Septemba 1988. Kwa mujibu wa wakili, umiliki huo ulikuwa wa miaka 33 kutoka mwaka huo wa 1989 na 1988.
Baada ya wateja wa wakili Boniface kununua mashamba hayo, walifuata taratibu zote za kisheria ikiwemo kufanya uhamisho wa miliki (transfer) na kulipa kodi stahiki. Hatimaye umiliki ulipasishwa na kuhamishwa rasmi kwenda kwa familia ya Ismail Thakore, ambayo inajumuisha Ismail Thakore, Suhel Thakore na Isihaka Thakore. Familia hiyo inatajwa kuwa wamiliki halali wa shamba hilo kwa mujibu wa hati kwa miaka 99 iliyotolewa tarehe 20 Januari 2023.
Aidha, wakili Boniface alibainisha kuwa hatua zote za kufuatilia uhakiki wa miliki pamoja na ulipaji wa kodi za halmashauri zilifanywa ipasavyo, na mamlaka za ardhi ikiwemo Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Iringa walithibitisha umiliki huo bila shaka.
Hata hivyo, chanzo kikuu cha mgogoro huo, kwa mujibu wa wakili, kinadaiwa kuwa ni baadhi ya viongozi wa kijiji husika ambao wamekuwa wakishiriki kuuza maeneo ndani ya shamba hilo bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesema viongozi hao wamekuwa wakifanya mauzo holela bila kujiridhisha kupitia ofisi za ardhi kama maeneo hayo yana mmiliki mwingine au la.
Katika siku za karibuni, wakati wa zoezi la upimaji wa mipaka, idadi kubwa ya wananchi walijitokeza kudai kuwa maeneo hayo ni mali yao.
Wakili anasema historia inaonyesha kuwa kabla ya Operesheni Vijiji ya mwaka 1978, wananchi hao waliwahi kuishi kwenye maeneo hayo lakini walihamishwa na Serikali ili kupisha utekelezaji wa sera ya vijiji vya kisasa na kutoa huduma bora zaidi.
Licha ya kwamba maeneo hayo yalishahamishwa na kupangiwa matumizi mapya ya kilimo, baadhi ya wananchi bado wamekuwa na imani kuwa ardhi hiyo ni mali yao ya kihistoria. Hata hivyo, wakili Boniface anasema elimu inaendelea kutolewa na wengi wanaanza kuelewa taratibu za umiliki kihalali.
Wakili Inno Boniface anasema kuwa awali tulikuwa na kesi dhidi ya kampuni hiyo na shirika la Saint Dominic Savio wao walikuwa wakilalamika kumiliki sehemu ya hilo eneo takribani hekta 300 ambapo walikaa mezani na kupeana nyaraka za uhalali wa umiliki wa kampuni ya Iringa Food and Beverages Ltd na wao kulidhia kuachana hilo eneo kwa makubaliano hii kutokana na kuuziwa na wanakijiji wa pale na serikali ya kijiji ikabariki kwa kupewa hati miliki za kimila hivyo kiutaratibu huwezi kuwa na hati ya kimila kwenye hati kubwa na hiyo baada ya kufikishana mahakamani.
Anaongeza kuwa kwa sasa kuna kesi ambayo mtu mwingine katika eneo hilo hilo ambalo walikuwa na mgogoro na Saint Dominic Savio ambaye naye anasema anamiliki eneo hilo kwa ekari 30 na kesi imeenda mahakamani ambapo itakuwa tarehe 5 mwezi 5 mwaka huu katika baraza la ardhi la wilaya ili kwenda kuthibitisha kile ambacho kitapelekwa mahakamani.
Mgogoro huo unaendelea kufanyiwa kazi na mamlaka husika huku wamiliki wakisisitiza kuwa wanaamini sheria itasimama upande wa haki.






No comments:
Post a Comment