HABARI MSETO (HEADER)


 


Breaking

June 11, 2026

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA SLOVAKIA AWASILI TANZANIA KWA ZIARA RASMI YA KIKAZI

Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Jamhuri ya Slovakia, Mheshimiwa Juraj Blanár, amewasili katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ziara rasmi ya kikazi kuanzia tarehe 10 hadi 11 Juni 2026. Ziara hiyo inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Slovakia.



Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Blanár alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa James Millya (Mbunge).

Katika ziara yake, Mheshimiwa Blanár anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mbunge), tarehe 11 Juni 2026. Mazungumzo hayo yataangazia namna ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, elimu, programu za ufadhili wa masomo, usalama wa mtandao, biashara na uwekezaji.

Baada ya kikao hicho cha pande mbili, Mawaziri hao wawili watazungumza na vyombo vya habari kabla ya kushiriki kwa pamoja katika uzinduzi rasmi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Slovakia jijini Dar es Salaam. Ubalozi huo, ambao ulianza rasmi shughuli zake mwezi Novemba 2025, unaonyesha dhamira ya pamoja ya Tanzania na Slovakia ya kuimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia na kupanua ushirikiano katika maeneo ya uchumi na maendeleo.

Mheshimiwa Blanár ameambatana na takribani wafanyabiashara 50 watakaoshiriki katika Kongamano la Biashara la Tanzania na Slovakia. Kongamano hilo litawakutanisha viongozi wa biashara na wawakilishi wa sekta binafsi kutoka nchi zote mbili kwa lengo la kujadili maeneo mapya ya ushirikiano na ubia wa kibiashara.

Kongamano hilo linatarajiwa kuchunguza fursa za biashara na uwekezaji, kuhamasisha uhamishaji wa teknolojia, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati zikiwemo nishati jadidifu, uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na ubunifu wa kidijitali.

Ziara hii inaonesha dhamira ya pamoja ya Tanzania na Slovakia ya kuendeleza uhusiano wa pande mbili na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.

No comments:

Post a Comment

Pages