NA EDITHA WILLIAM -KAGERA
Wanandoa Mkoani Kagera wameshauriwa kuishi kwa upendo na amani ili kuepuka kuleta migogoro katika familia inayoweza kuleta utengano kwa watoto.
Hayo yamebainishwa na wadau mbali mbali katika kikao cha tathimini ya utekelezaji wa majukumu ya ulinzi na usalama wa mtoto kilichofanyika katika ukumbi wa vijana kata ya Kyaka Wilaya Missenyi Mkoani Kagera kilichoongozwa na wawezeshaji kutoka katika kituo cha Tumaini children center kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kinachohudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi mitaani
Aidha, wadau hao wamesema kuwa wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuwapatia msaada wa kisaikolojia, ushauri na kuwapatia mahitaji muhimu ili kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama wao katika jamii pamoja na kupata haki zao za msingi
Sambamba na hayo, pia wameeleza baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na uaminifu, ushirikishwaji, uelewa hafifu, upungufu wa vitendea kazi, kutokujiamini pamoja na hofu
Hata hivyo wamependekeza kamati za ulinzi na usalama wa mtoto kujengewa uwezo wa mara kwa mara, kutoa elimu kwenye nyumba za ibada, mashuleni pamoja na kwenye mikutano ili kuhakikisha ulinzi wa mtoto na usalama wake unaimarishwa
Tumaini Johanes Bahati na Jovice Denice ni watoto walioshiriki katika kikao hicho wameeleza mchango wao wa ushawishi kwa watoto wenzao kuhakikisha wanakwenda shule kupata elimu bora ili kuepuka kubaki mitaani
Kwa upande wake Jovith Paschal ambae ni Mwezeshaji wa kituo cha Tumaini Chidren Center amesema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuepuka unyanyasaji uliokithiri kwenye familia kwani imetajwa kuwa sababu kubwa ya watoto kutoroka nyumbani na kukimbilia mitaani na kusema kuwa ni lazima mtoto ajengwe kisaikolojia katika makuzi yake
Kituo cha Tumaini Children Center kilianzishwa mwaka 2003 kikiwa na lengo la kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi mtaani





No comments:
Post a Comment