Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea
kuimarisha juhudi za kuhakikisha kuwa masuala ya uendelevu wa mazingira
yanapewa kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi
Hamad Yussuf Masauni, aliposhiriki matembezi yaliyolenga kuhamashisha jamii
katika Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira ‘Save Soil Walkathon’ yaliyofanyika
Julai 19, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mhe Masauni
amesema, ahadi hii
inaonyeshwa wazi katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050, haswa nguzo yake
ya Tatu, ambayo inatambua uendelevu wa mazingira na ustahimilivu wa hali ya
hewa kama misingi muhimu wa kufikia mabadiliko ya kiuchumi jumuishi ya kijani
kibichi na endelevu.
Ameongeza kuwa afya ya udongo ni msingi wa usalama
wa chakula, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa uchumi wa taifa, hivyo kuna
umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki katika juhudi za kuutunza.
"Udongo ni
rasilimali muhimu inayobeba maisha yetu ya kila siku. Bila udongo wenye afya
hatuwezi kuwa na usalama wa chakula, mazingira bora wala maendeleo endelevu. Ni
wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika juhudi za kulinda mazingira na
kutumia ardhi kwa njia zinazohifadhi uhai wake kwa manufaa ya kizazi cha sasa
na kijacho," amesema Mhe. Masauni.
“Tunapoanza kutekeleza Mpango huu wenye kuleta mabadiliko makubwa, tunaona
fursa nyingi za kuimarisha ushirikiano wetu na Jamhuri ya India. Tunatarajia
kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama vile uhamishaji wa
teknolojia, utafiti na uvumbuzi, ujenzi wa uwezo, urejeshaji endelevu wa ardhi,
ufuatiliaji wa mazingira, uwekezaji rafiki kwa mazingira na suluhisho
zinazozingatia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.” Amesisitiza Mhe.
Masauni.
Kwa upande wake,
Rais wa Lions Club of Dar es Salaam Mazingira, Bi. Lion Ramadevi, amesema ‘Save
Soil Walkathon’ ni sehemu ya kampeni pana inayolenga kuhamasisha jamii kutambua
mchango mkubwa wa udongo katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.
"Save Soil
Walkathon si matembezi pekee, bali ni harakati ya kuhamasisha mabadiliko ya
tabia na kuwajengea wananchi uelewa wa umuhimu wa kulinda udongo. Tunataka
kuona jamii, taasisi na sekta binafsi zikichukua hatua za pamoja katika
kuhifadhi mazingira kwa mustakabali wa taifa letu," alisema Lion Ramadevi.
Naye Balozi wa
India nchini Tanzania Mhe. Lakshay Anand
amesema ni jambo jema kuona jamii inatambua umuhimu wa kulinda mazingira na huo
ndio msingi wa Maisha ya binadamu ya kuhakikisha kila mmoja anakua sehemu ya
kutunza mazingira.







No comments:
Post a Comment