Emmanuel Adebayor
LOME, Togo
RAIS wa Togo, Faure Gnassingbe ameitisha kikao maalum baina
yake na nahodha wa timu ya taifa ya hapa, Emmanuel Adebayor – baada ya mkali
huyo kukataa kujiunga na kikosi hicho kwa ajili ya fainali za mwezi huu za
Mataifa Afrika (AFCON 2013) kushinikiza ongezeko la bonasi inayotolewa na
Shirikisho la Soka.
Waziri wa Michezo wa hapa, ameyasema hayo na kuongeza kuwa
Adebayor anayechezea klabu ya Tottenham Hotspur ya England, anatarajia kuwasili
jijini hapa wakati wowote kuanzia leo, tayari kwa mazungumzo hayo Ikulu na mkuu
huyo wa nchi ambayo yametabiriwa kubadili msimamo wa nyota huyo.
Togo leo Jumamosi anatarajiwa kuumana na Niger jijini Niamey,
ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kwa ajili ya AFCON 2013, michuano
inayofunguliwa rasmi Januari 19, nchini Afrika Kusini.
Kiungo-mkabaji wa timu hiyo, Alaixys Romao anayekipiga soka
la kulipwa nchini Ufaransa akiwa na klabu ya Lorient, alibadili msimamo na
kukubali kujiunga na kambi ya timu hiyo katikati ya wiki, baada ya awali
kuungana na Adebayor kujitoa katika kikosi kilichokuwa kikijiandaa kwenda
AFCON.
Kipa chaguo la kwanza wa kikosi hicho, Kossi Agassa amekataa
pia kuitikia mwaliko wa kocha Didier Six wa kujiunga na Togo kwa ajili ya
fainali hizo, akisema ataendelea kusubiri kujua ufumbuzi wa madai ya msingi ya Adebayor
yatakapotatuliwa.
Togo inatarajia kufungua pazia la michuano hiyo kwa kuumana
na washindi wa pili wa fainali zilizopita Ivory Coast, ikiwa ni mechi ya kundi D
litakaloungurumisha mechi zake huko Rustenburg.
No comments:
Post a Comment