WAKATI Manchester City ikijiandaa
kupungukiwa nguvu kwa nyota wake Yaya na Kolo Toure kutarajia kujiunga na timu
ya taifa itakayoshiriki fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2013), imepata pigo
kwa mshambuliaji wake Sergio Aguero (Pichani juu) kuumia.
Aguero nyota wa kimataifa wa
Argentina, alipata majeraha na ameripotiwa kuwa na uwezekano wa kukaa nje ya kikosi
kwa wiki mbili hadi tatu, baada ya kuumia misuli wakati mabingwa hao watetezi
wa Ligi Kuu wakishinda 3-0 dhidi ya Stoke City Jumanne jioni.
Mkali huyo alilazimika
kutolewa nje ya dimba baada ya kufunga mkwaju wake wa penati katika dakika ya
74, kukinyanyua juu kikosi cha Roberto Mancini kilichopata ushindi huo muhimu.
Man City ilikuwa na matarajio
ya kumkosa Aguero katika kipindi cha wiki moja, lakini msaidizi wa Mancini,
David Platt amedokeza kuwa nyota huyo hatukuwapo dimbani kwa muda, akitarajia
kulikosa pambano la raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Watford Jumamosi.
Aguero, ambaye alikuwa
mfungaji bora wa Man City msimu uliopita, akikumbukwa kwa bao la dakika za lala
salama dhidi ya QPR lililoipa ubingwa wa Ligi Kuu, pia atalikosa pambano kali na
la kukata na shoka dhidi ya Arsenal hapo Januari 13.
"Kwa sasa ni vigumu
kutathmini kiwango gani Aguero ameumia na atakuwa nje ya dimba kwa muda gani,"
alisema Platt.
"Tuna uhakika ya yeye
kukosa pambano la Jumamosi dhidi ya Watford, lakini pia uzoefu wangu unanipa
shaka ya kuweza kuiwahi mechi dhidi ya Arsenal. Lakini kuna viwango tofauti vya
maumivu ya misuli, ndio maana tunahitaji kujua hilo baada ya saa 48.
"Kuna aina nyingi za
maumivu ya misuli nah ii hatujaijua hadi vipimo ambavyo ndivyo tunasubiri.
"Kumekuwa na aina kibao
za majeruhi zikiwamo za kuvimba na ile ya kutokwa na damu kwa ndani. Hatujui
hii ni ya aina ipi na utamchukua muda gani," alimaliza Platt.
Kuumia kwa Aguero na kuondoka
kwa familia ya Toure kunazua shaka katika kikosi cha Man City, ambacho kwa sasa
kiko nyuma kwa pointi saba katika jaribio la kutetea ubingwa wao, ulio hatarini
kuporwa na vinara Manchester United.
No comments:
Post a Comment