HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 15, 2013

Askofu Amani: Tumeingiliwa na saratani ya uvunjifu wa amani

Askofu wa Jimbo la Moshi la Kanisa Katoliki Tanzania, Askofu Isaac Amani Massawe amesema kuwa Tanzania imeingiliwa na ugonjwa wa saratani wa kuvunja amani na utulivu na Watanzania wasipobalika na kukubatia amani watajuta.
Amesema kuwa baada ya miaka 50 ya Uhuru, Watanzania sasa wamefungua ukurasa mpya na nchi imeanza kupoteza sifa ya kuwa nchi ya amani na utulivu.
Aidha, amesema kuwa wajibu wa watu kuishi kwa amani siyo wajibu wa Serikali ama wa Dini ama wa Kanisa bali ni wa kila mtu kwa nafsi yake.
Askofu Amani ameyasema hayo leo, Alhamisi, Februari 14, 2013 wakati alipokuwa anatoa neno la shukurani baada ya kumalizika kwa Ibada ya Mazishi ya aliyekuwa Askofu Jimbo la Moshi, Askofu Mstahivu Amedeus Peter Msarikie katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme mjini Moshi.
Askofu amewaambia mamia kwa mamia ya waumini: “Tumefungua ukurasa mpya katika Tanzania. Baada ya miaka 50 ya amani na utulivu sasa tumebadilika. Tanzania ya leo siyo Tanzania ya zamani sasa tumeanza kuongozwa na misingi ya vurugu za kidini na vurugu za kifedha.”
Ameuliza Baba Askofu Amani: “Tumeelimika zaidi ama tumechoka amani? Tumeingiwa na saratani ya uvunjifu wa amani na migawanyiko kwa misingi ya kidini na kifedha na mingine ya aina mbali mbali. Njia nzuri ya kuagana na mzee wetu Askofu Msarikie ni kuishi maisha aliyoishi yeye- maisha ya amani na utulivu. Yeye alikuwa chombo cha amani na anapumzika kwa amani kwa sababu aliishi maisha ya amani.”
Ameongeza: “Kuishi kwa amani na utulivu siyo suala wala wajibu wa Serikali ama wa Kanisa ama wa Dini ni wajibu wa kila mtu kwa nafsi yake na kila mmojawetu anao wajibu wa kusali ili kuombea amani ambayo imedumu katika nchi yetu kwa miaka mingi sana – miaka 50 sasa lakini inaonyesha kila dalili ya kutoweka.”
Amesisitiza: “Ndugu zangu amani hairithishwi, amani hujengwa na hulindwa. Changamoto alichotuachia Askofu Msarikie ni kutafuta na kuilinda amani katika nchi yetu. Huwezi kuwa mtu wa vurugu na mvunja amani na bado ukapata starehe ya milele mbele ya Mwenyezi Mungu. Sasa ni wakati wa kulea taifa letu, kulitengeneza upya na tumwombe Mungu atusaidie katika safari hii ndefu.”

No comments:

Post a Comment

Pages