HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 15, 2013

Ningekuwa Shonza ningekaa kimya!!


 ‘Mbaazi ikikosa maua husingizia Jua!

Na Bryceson Mathias

NI hivi karibuni Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), lilisema limemvua uanachama aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Juliana Shonza baada ya kubainika alikuwa akifanya vikao vya siri kukisaliti chama hicho akishirikiana na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Pamoja na Shonza kuwa Msemaji sana wa kutaka kushindana na kujionesha, lakini ningekuwa mimi ndiye yeye ningenyama kimya ili ili nihesabiwe Hekima na ningefunga midomu yangu ili nihesabiwe ufahamu ieleweke si kwamba kusema hivyo nakurupuka la hasha; ujanja huo uko kwenye maandiko ya Dini Mithali 17:28.

Kama kuna andiko ninaloliogopa nikiwa Mkristo kama alivyo Shonza, basi ni la kuwatukana au kuwakashifu wazazi Baba na Mama yaani watu waliokuzidi Umri wakikushauri, kama inavyodaiwa alikuwa akifanya Shonza dhidi ya Katibu wa Chadema Dk. Wilbrod Slaa.

Andiko hilo ninaloliogopa liko kwenye Kitabu cha Mathayo 15:4 – Kwa kuwa Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na Amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe”.

Kumbe kimsingi tukiwa tunawakashifu watu wazima waliotuzidi umri wanaopaswa kutushauri tusiingie mahali pabaya kiasi cha kutusababishia vifo hata ka kama si vya mwili bali vya kiasa, tunajiweka mahali pabaya ambapo Laana hizo zinapotukuta tunadhani tumerogwa au kufanyiwa uganga kumbe tumelaaniwa na Mungu kwa kukosa adabu.

Sijaelewa Shonza alikuwa wapi nilipowaonya vijana kwa makala yangu ya Vijana wasikubali kufanywa kuwa Karai la nzege. Karai hubeba nzege tangu nyumba inapoanza kwenye msingi hadi ghorofa ya 10 na kuendelea, lakini siku ikimalizika Karai hutupwa nje kama Uchafu na kutofaidi juhudi za ushiriki wake katika Ujenzi.

Nina uhakika Shonza analingana na Mwanagu niliyemza. Hivyo Napata mashaka kwamba, mbwembwe anazofanya za kujisahau na kufunua kinywa kwa matamko yasiyo na Hekima na pengine kuchanganywa na akili za wanaomdanganya ili wamtumie vibaya. Zinakumaliza kisiasa, na baadaye utakosa kuaminika hata huko ulikohamia.

Hao hao wanaojifanya kuwa wanakupenda sasa unapowatekelezea kazi zao, ipo siku watakwambia kama uliweza kusema machafu na yasiyo ya kweli ukiwa chadema, watahofu kwamba hata huko kwao utakapodanganyika na kukutumia vbaya kama chombo cha kuwapa umaarufu, wakiupata watakutupa kama Karai.

Ni rai yangu kukukumbusha kwamba, kama ulivyosoma shule na kuelewa maana ya Usiache Mbachao kwa Msala Upitao!! Ipo siku utayakumbuka maneno haya.
Siri ya Jeshi ukiende kufanya Uchunguzi halafu ukakamatwa au kubainika na Adui.cha kwanza hutakiwi kusema Siri za Jeshi uilo lako. 

Hata Mwananmke au Mwanaume wakikosana na Mwenzi wake halafu akaanza kusema madhaifu ya mwenzake mbele ya watu, watu humtafsiri kuwa yeye ndiye ana tatizo ndiyo maana kinywa chake kiko wazi.

Hata mimi niliyedhani labda unaonewa , sasa nimekubaini kuwa ulikuwa na matatizo kwa sababu ya kushindwa kutulia katika mambo yako kukiwepo kuropoka ropoka ovyo kwenye vyombo vya habari na popote unapopata nafasi ya kuongea.

Waswahili ambao wamebobea katika mambo ya Wenzi yaani wenye Ndoa, humshangaa sana Mwanamke au Mwanaume , mwenzake akifariki kabla hata wiki haijaisha anakuwa amepata mtu wa kumuoa au kuolewa. Kimsingi hata ujitete vipi kwao watakung’ang’ania kuwa huo umpendaye ulikuwa naye hata kabla mwenzako hajafariki na hivyo ulikuwa unamuibia au kumkiuka.

Mfurukutwa mmoja wa Chadema alisema hivi, “Sababu za kufukuzwa kwa Shonza  ambazo Chadema iliainisha kupitia viongozi wake ziliainishwa vizuri sana, hao wanataka maelezo zaidi wafanywaje? Walitaka aendelee kufanya kazi ya CCM akiwa amejivika magwanda ya CHADEMA? Sasa wamepewa uhuru wakafanye hiyo kazi  huko huko”

Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema Shonza alikuwa akiwashawishi wenzake kuitisha mikutano na waaandishi wa habari kumkashifu Katibu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa.

“Aende CCM hapa tumemng’oa kwa sababu alikuwa kirusi hatari kwa chama, alikuwa Chadema huku akifanya kazi na CCM, tuna ushahidi wa picha, mikanda ya video na jumbe za simu za mikononi,” alisema Heche.

Licha ya kumfuta uanachama Shonza, baraza la vijana pia lilimewavua uanachama Habib Machange aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Kibaha Mjini na Mtela Mwampamba aliyegombea ubunge Jimbo la Mbozi Mashariki.

Heche alituhabarisha kuwa  makamu wake alikuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya baraza hilo, chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko.

Ilidaiwa pia, alikuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa manufaa ya CCM, akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni ili kuikashifu Chadema na viongozi wake wakuu.

Kuhusu Mchange, Heche alitujuza kuwa huyo alivuliwa uanachama kwa kutoa tuhuma za uongo ikiwamo mauji, kinyume na maadili ya wanachama na kuunda vikundi vinavyojulikana kama masalia na PM7-Pindua Mbowe.

Alisema Mchange alituhumiwa na kuwavuruga wanachama, kuwachonganisha na kuwatukana viongozi kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha siasa cha Chauma, ambapo kwa upande wa Mwampamba, alisema alikuwa akitoa tuhuma nzito za uongo hadharani ikiwamo za mauaji.

Alisema mwanachama huyo kama alivyo mwenzake alishiriki vikao vya kuanzisha chama cha siasa cha Chaumma akiwa Chadema.

Heche aliongeza kusema, Ben Saanane, huyo alipewa onyo kali baada ya kukiri kujiunga na vikundi vya masalia na PM7 na kwamba, kwa sasa amepewa miezi 12 ya uangalizi ili ajirekebishe.

Aidha kipindi kama hicho kilitolewa kwa Gwakisha Mwakasendo aliyetenda makosa ya kushiriki vikao na vikundi hivyo na kwamba, alikiri kosa na kupewa onyo kali, naye atakuwa kwenye uangalizi kwa miezi 12, ambapo Suala la Exaud Mamuya halikusikilizwa, hivyo litaendelea kufanyiwa kazi na uongozi wa Bavicha

Ingawa Shonza mjini Dodoma alikabidhiwa kadi yake ya CCM na Mwenyekiti wa CCM, taifa, Rais Jakaya Kikwete, amekuwa kama Kuku Mgeni ndani ya CCM ambaye bado ana Kamba Mguuni, huku akiwafanya wanaompokea kuwa na mashaka naye iwapo kuku huyu ana Kideli au La?

Akizungumza mbele ya Kikwete, Shonza alidai amefanya uamuzi huo kutokana na CHADEMA kukosa Demokrasia. Maneno hayo ni ya Sungura pamoja na ujanza wake alipozikosa ndizi zilizoko juu ya mti kutokana na ufupi wake alisema Mbichi wakati zimeiva.

Aliilalamikia CHADEMA kuwa imekithiri kwa ufisadi, lakini imekuwa mstari wa mbele kuzungumzia ufisadi wa CCM. Je yeye hauelewi Ufisadi aliokuwa akiifanyia Chadema hadi ikamng’amua? Ulikolalia wewe ujue ndiko wenzako walikoamkia.

Aidha alisema ndani ya CHADEMA kuna mfumo dume na kwamba hakuna mwingine anayetoa kauli zaidi ya viongozi wa juu wa chama hicho! Kati hilo simuamini hata kidogo maana kungekuwa na Mfumo Dume yeye asingekuwa kiongozi hadi alipojichafua.

Shonza alitumia fursa hiyo kumtumia salamu Mbunge wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA) na kumtaka ajiandae kwa mapambano katika uchaguzi wa mwaka 2015, jambo ambalo wadau wa siasa wanasema kama alitumwa kwa ajili yake amemkosa asubiri mvua inyeshe ila sasa kwake ni kiangazi.

Hata hivyo kwa upande wake Mwampamba alisema amejiunga na chama hicho kwa hiari yake mwenyewe bila kushinikizwa na mtu yeyote, Rais Kikwete ambaye ndiye aliyetoa kadi za CCM kwa vijana hao, aliwapongeza kwa kuamua kujiunga na chama hicho tawala.

Ninyi vijana kwa nini mnatukana Wakunga na Uzazi Ungalipo? hizo ndiyo Hasara zake. ningekuwa Shonza, ningenyamaza Kimya!!! ili nisiaibike.om


0715-933308

No comments:

Post a Comment

Pages